HUDUMA za matatibu kwa mfumo wa Hospitali Tembezi iliyoanza Jumatatu Juni 25, 2018 inaendelea katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Dodoma Mtakatifu Gemma iliyopo Kata ya Miyuji Jijini humo ambapo mpaka sasa jumla ya wagonjwa 664 wamehudumiwa ndani ya siku mbili za Jumatatu na jumanne.
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Ernest Njile, Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali wamekutana pamoja kutoa huduma za kiwango cha hali juu ambapo kati ya wagonjwa 664 waliohudumiwa, wagonjwa 26 wamefanyiwa upasuaji wa mifupa na wa kawaida na zaidi ya wagonjwa 38 wanatarajiwa kupasuliwa leo Jumatano Juni 27.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma hiyo Hospitalini hapo leo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI Selemani Jaffo aliipongeza Halmashauri ya Jiji na wadau wote kwa kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa Afya za Watanzania na kwamba huduma wanayoitoa ni ya kujitoa na ni ibada kubwa mbele ya Mungu.
Alisema kuwa, amepita katika wodi mbalimbali na kushuhudia wagonjwa wanavyopatiwa huduma ambapo baadhi yao walikuwa wamekata tamaa ya kupata matibabu lakini wamepata matumaini mapya baada ya kusogezewa huduma hiyo ya kibingwa.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alitoa wito kwa wananchi hususan wakazi wa Jiji kujitokeza kupata huduma hiyo iliyosogezwa karibu zaidi, ikiwa ni juhudi za Serikali za kuwafikishia Wananchi wake huduma.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji hilo Profesa Davis Mwamfupe awataka madiwani wenzake kuhamasisha Wananchi katika Kata zao ili wajitokeze kwa wingi kupatiwa huduma za Afya na wataalam hao waliobobea.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Ajira ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde aliiomba Serikali kupitia kwa Waziri Jaffo kulipatia Jiji la Dodoma fedha za ujenzi wa kituo cha Afya katika Kata ya Miyuji ili kisaidie kuhudumia wagonjwa wengi wanaotegemea Hospitali Teule ya Wilaya Mtakatifu Gemma.
Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma Hamadi Nyembea alisema huduma hiyo inafanikishwa na Jiji kwa kushirikiana na Hospitali mbalimbali ikiwemo Benjamini Mkapa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, na inatarajiwa kuendelea hadi Ijumaa Juni 29, 2018.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.