Takribani miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake, Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyoko Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Jijini Dodoma, imeonyesha kupata mafanikio makubwa katika utoaji huduma bora za afya ndani ya muda mfupi.
Hospitali hii ya Benjamin Mkapa, ilianzishwa mwaka 2015 kwa tamko la Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na ilizinduliwa rasmi Oktoba 13 ya Mwaka huo huo.
Lakini ndani ya muda huo mfupi wa miaka mitatu, Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambayo inatajwa kuwa tegemeo la nchi, imeweza kutoa huduma mbalimbali za kiafya zikiwa na ubora wa hali ya juu na zingine zikiwa ni nadra kupatikana ndani ya ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Akielezea mafanikio hayo ya muda mfupi, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya wadhamini ya Hospitali hiyo hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika amesema tangu kuanzishwa kwake, hospitali imekuwa na mafanikio makubwa sana.
“Wigo wa huduma katika hospitali hii tangu kufunguliwa kwake umeendelea kukua kila kukicha, haya ni mafanikio makubwa na ya kujivuni”, alisema Dkt. Chandika.
Dk. Chandika alisema ndani ya miaka miwili tu mpaka Juni, 2017, hospitali hiyo ya Benjamin Mkapa tayari ilikuwa imeshafungwa mitambo ya uchunguzi wa maradhi kama ya MRI, CT-Scan, Fluoroscopy, Mammography, huduma za mionzi (X-ray) na Endoscope.
Dk. Chandika amesema ya kuwa mitambo hiyo ni ya kisasa na mingine ikiwa inapatikana hapo Hospitali Benjamin Mkapa tu hapa nchini.
“Mitambo hii ni ya kisasa na inatumia teknolojia ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kutambua maradhi, mfano MRI ilyopo hapa yenye ukubwa wa 3T na kwa hapa nchini ipo Hospitali ya Benjamin Mkapa tu na inawezekana ikawa hivyo hata Afrika Mashariki nzima, “alisema Dk. Chandika.
Dr. Chandika aliongeza, “Vifaa vya Endoscopy vimemalizika kufungwa Mei mwaka huu katika vyumba 6 vya upasuaji na ni vya teknolojia ya hali ya juu ambapo vimeunganishwa na mfumo wa tibamtandao (Telemedcine) ambapo itawezesha mtaalamu aliyeko hapa kushauriana na mtaalamu aliyeko Dar es Salaam na hata nchi za nje wakati wa kufanya upasuaji”.
Aidha, Dk. Chandika amesema Hospitali hiyo imekuwa ikitoa huduma za kawaida na za kibingwa kama vile magonjwa ya ndani (internal medicine), watoto (pediatrics) upasuaji, afya ya uzazi na kizazi, upasuaji wa njia ya mkojo, upasuaji wa koo, pua na masikio.
Kwa upande wa huduma za kibingwa, Dk. Chandika alisema hospitali hiyo inatoa huduma ya matibabu ya maradhi yanayoathiri mfumo wa kumeng’enya chakula tumboni mwa binadamu (Gastroenterology), matibabu ya saratani kwa kutumia drip kwa watoto, upasuaji wa tezi dume.
Huduma zingine ni usafishaji wa damu kwa wagonjwa ambao figo zao hazifanyikazi, pia huduma za upandikizaji figo ambao hospitali hii imekuwa ya pili nchini kuianzisha baada ya Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili.
Wakati huohuo, Dk. Chandika alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa Madaktari Bingwa ambao kwa sasa wapo 12 tu huku wakihitajika Madaktari 40 hospitalini hapo.
Changamoto zingine, alisema ni pamoja na upungufu wa nyumba za watumishi wa hospitali hiyo na usafiri kwa watumishi hao kutoka mjini mpaka eneo la hospitali lilioko nje ya Mji wa Dodoma.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Ally Mwalimu, akihutubia kwenye hafla hiyo, alisema ya kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ni mkombozi kwa Taifa dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo husababisha vifo vingi.
“Takwimu zinaonyesha ya kwamba, magonjwa yasiyo ya kuambukiza husababisha vifo vingi duniani kote kuliko yale ya kuambukiza, kwa bahati nzuri hospitali ya Benjamin Mkapa ilianzishwwa mahususi kutoa huduma za kibingwa katika maeneo hayo na sote tunashuhudia ya kwamba, tayari huduma hizo zimeanza kutolewa na mfano hai ni zoezi la kwanza lililofanyika hapa hospitali, Machi Mwaka huu la upandikizaji wa figo”, alisema Waziri Ummy Ally Mwalimu.
Pia, Waziri huyo alisema ya kuwa ana imani kubwa ya kwamba hospitali hiyo ambayo kwa sasa inatoa huduma za matibabu ya figo na moyo itasaidia kuipunguzia Serikali gharama kubwa za matibabu hayo zilizokuwa zikitolewa nje ya nchi.
“kuanzishwa huduma hizi za matibabu ya moyo na figo katika hospitali zetu ikiwemo Hospitali ya Benjamin Mkapa kutaokoa kiasi kikubwa sana cha pesa na kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa gharama na badala yake pesa hizo zilizookolewa zitatumika kuimarisha miundombinu ya hospitali zetu kote nchini” alisema.
Aidha, Waziri aliushukuru Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kugharamia ujenzi wa majengo mawili ya hospitali ya Benjamin Mkapa ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa tiba uliogharimu shilingi bilioni 119.2.
Kuhusu utafiti, Waziri huyo aliitaka Hospitali ya Benjamin Mkapa ijikite zaidi katika utafiti akisema zinasaidia, pamoja na mambo mengine ikiwemo kuongeza maarifa ya kupambana na magonjwa.
“Tafiti ni eneo nyeti na muhimu sana katika kukuza na kuendeleza weledi, ujuzi na maarifa katika taaluma mbalimbali, tafiti hizi ni muhimu katika kuongeza uwezo wa kupambana na magonjwa hivyo, ni lazima Hospitali ijikite katika kufanya tafiti mbalimbali ilikugundua matatizo, changamoto na kuyapatia majawabu kwa maendeleo ya hospitali na Taifa kwa ujumla,” alisisitiza Waziri.
Waziri huyo aliwaomba watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii katika kuwatumikia wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali hiyo, Dkt. Deodatus Mtasiwa, aliishukuru Serikali kwa kuwateua wao kuwa wajumbe wa kwanza wa Bodi hiyo ya wadhamini huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo katika Hospitali hiyo.
Malengo ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Hospitali hiyo ya Benjamin Mkapa Mkoani Dodoma, ilianzishwa kwa lengo la kutoa huduma za Afya Maalum za Kibingwa (Specialized and Super-specialized Services), huduma za uchunguzi na tiba kwa magonjwa yote huku ikijikita zaidi kwenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama maradhi ya figo, moyo, macho, damu, saratani na kadhalika pamoja na kutoa huduma za kifaa maalumu cha kuchunguza maradhi ndani ya mwili wa binadamu kinachojulikana kitaalamu kama endoscope.
Pia, kufundisha wataalamu wa kada mbalimbali za huduma za afya na kufanya tafiti mbalimbali ili kuboresha afya ya jamii ya Watanzania na hivyo kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama za matibabu nje ya nchi.
Chanzo: Jarida la Dodoma Yetu
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.