Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara (Kwangwa) iliyoasisiwa na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1977 imeanza kutoa huduma ya magonjwa ya nje (OPD) na kitengo cha Mama na Mtoto. Hii inafuatia Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufanya ziara katikati ya mwezi huu na kuitaka Hospitali hiyo kuanza huduma mara moja baada ya ujenzi wake kuwa umefikia zaidi ya asilimia 90.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo tarehe 31 Agosti, 2020 imesema kuwa Wazara inafurahi kuujuza umma kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara (Kwangwa) imeanza kutoa huduma za matibabu ikiwa ni utekelezaji wa adhma ya muda mrefu ya Serikali kuendelea na utekelezaji wenye lengo la kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.
Matokeo ya kuanza kwa huduma yameleta matunda na matokeo chanya katika siku ya kwanza ya utoaji huduma hospitalini hapo, ambapo hadi mchana watoto watatu wamezaliwa salama salmini na wote wakiwa na afya njema pamoja na wazazi wao.
Watoto hao watatu ambapo aliyezaliwa wa kwanza ni wa kiume na wawili wengine waliofuata ni wa kike wamepewa na wazazi wao majina ya Julius, Maria na Samia kwa heshima za viongozi wetu pamoja na kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere, mke wa Baba wa Taifa, Mheshimiwa Mama Maria Nyerere na Makamu wa Rais Mheshimiwa Mama Samia S. Hassan.
Ikumbukwe, Hospitali hii (Mwalimu Nyerere Memorial Regional Referral Hospital) ni moja kati ya Hospitali za Rufaa za Mikoa 10 zinazojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ambayo ujenzi wake ulikwama tangu miaka ya 1970 na sasa imeanza kutoa huduma kwa maeneo ambayo yamekamilika yaliyochagizwa na usimamizi madhubuti na ziara za mara kwa mara za ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma zinazofanywa na viongozi, Waziri, Katibu Mkuu, Mganga Mkuu wa Serikali na Menejimenti ya Wizara kwa ushirikiano wa karibu na Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).
Mwonekano wa nje wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara (Kwangwa).
Tazama taarifa iliyotolewa siku za nyuma
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.