Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WILAYA ya Dodoma imemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ili kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma ilipotembelea na kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe.
Shekimweri alisema “hapa Dodoma hatuna hospitali ya wilaya, nichukue nafasi hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya pale Nala. Hatujaanza ujenzi sababu tumeomba idhini ya kujenga hospitali ya ghorofa. Nimshukuru Mganga Mkuu wa Jiji, Dkt. Andrew Method pamoja na wenzake hasa katika mazingira haya ambayo hatuna hospitali ya wilaya, Kituo cha Afya Makole kinafanya kazi kubwa kutusaidia kwa matibabu ya wagonjwa wa ndani”.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wameshapokea watumishi wa Afya 18. “Namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia watumishi wapya. Katika kituo hiki wameshapangwa watumishi 12, kwa hiyo, Mheshimiwa Diwani lile ombi lako kituo cha Afya kinakamilika hakina watumishi Rais Samia keshalijibu. Naomba muwapokee vizuri kama ulivyo mkarimu na wenzako muwapokee na kukaa nao kwa wema” alisema Shekimweri.
Akiwasilisha maelezo ya mradi huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt Andrew Method alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili. “Awamu ya kwanza tulipokea shilingi 250,000,000 zilizojenga jengo la wagonjwa wa nje, maabara na kichomea taka. Kazi imekamilika kwa 99%. Awamu ya pili tumepokea shilingi 250,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kina mama, jengo la upasuaji na jengo la kufulia. Ujenzi umeanza, tupo katika hatua ya msingi” alisema Dkt. Method.
Alisema kuwa ujenzi huo ukikamilika utahuduma wananchi karibu 30,000 waliokuwa wakizifuata huduma za afya Kituo cha Afya Makole. Alisema kuwa kituo cha Afya Makole kimekuwa na msongamano mkubwa wa wananchi wanaoenda kupata huduma hapo. “Tunatarajia kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi huu tarehe 29 baada ya kukamilisha uwekaji wa vifaa tiba na samani katika kituo hiko” alisema Dkt. Method.
Ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe ulianza tarehe 24 Desemba, 2021 kwa fedha za tozo kutoka serikali kuu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.