WANANCHI wa Kata ya Kikombo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kuchangamkia fursa ya matibabu ya kiwango cha juu yanayotolewa na madaktari bingwa katika kliniki tembezi inayolenga kuwafikia wananchi wengi wanaougua lakini wakishindwa kumudu gharama za kwenda maeneo ambayo wangeweza kupata huduma za madaktari mabingwa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi alipokuwa akizindua Kliniki Tembezi katika kituo cha Afya Kikombo kilichopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma jana.
Katambi alisema kuwa kliniki hiyo ni fursa kwa wananchi wa Kata ya Kikombo na kuwataka kuichangamkia. Alisema kuwa huduma hiyo itawaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Aidha, aliwataka kushirikiana vizuri na madaktari wa kituo hicho cha Afya ili waendelee kupatiwa huduma bora za tiba.
“Pongezi kwa kazi hii kubwa mnayoifanya, Dkt Gatete Mahava kazi hii ni kubwa sana na umefikiria jambo kubwa sana. Ni jambo la kukupongeza na inaonesha namna gani wewe ni shupavu sana kwenye eneo lako unalolisimamia kwenye idara ya Afya na kwa sababu kuna viongozi wa TAMISEMI hapa idadi ya makofi itakayopigwa hapa itakuwa inapeleka ujumbe kwa naibu katibu mkuu kwamba hawa watu wanastahili zaidi. Mungu awabariki sana na hongereni sana” alisema Katambi.
Mkuu huyo wa Wilaya aliwahakikishia wananchi kuwa timu ya madaktari iliyopo itafanya kazi kubwa na nzuri ya kibingwa. Serikali inaendelea kuboresha sekta ya Afya kwa lengo la kumhakikishia mwananchi Afya bora. “Maboresho katika sekta ya Afya yanakwenda kuakisi wale maadui watatu wanaosemwa ujinga, umasikini na maradhi. Na kwa kuondoa maradhi maana yake hakutakuwa na wajinga tena sababu watazaliwa watu wenye Afya bora” alisema Katambi. Dhamira ya serikali ni kunusuru wananchi wake wasiwe na magonjwa ya kuwazuia kufanya kazi na kukuza uchumi. “Hakuna maendeleo kama hakuna Afya bora kwa wananchi” alisema Katambi.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt Gatete Mahava alisema kuwa lengo la kliniki tembezi ni kutoa huduma zinazowavuta watu wengi kwa maana na kutafuta wagonjwa wenye magonjwa ambayo mara nyingi hayafahamiki na kuwapatia huduma za kibingwa katika maeneo yao.
“Tunatoa matangazo ya hamasa kwa lengo la kuwavuta wananchi kuja kupima na wanaokutwa na magonjwa mbalimbali wanapata matibabu ya kibingwa zaidi” alisema Dkt Mahava.
Kuhusu huduma zitolewazo katika kliniki hiyo, alizitaja kuwa ni tiba za kibingwa kwa magonjwa ya ndani, magonjwa ya kina mama, macho, upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi, afya ya uzazi na mtoto, hduuma za meno na kinywa na ushauri nasaha kwa watu wanaoishi na virus vya ukimwi. “Faida ya kliniki tembezi mpaka sasa hivi tumeona wagonjwa karibu 350 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6.30, lengo ni kuhudumia wagonjwa 500. Wagonjwa waliopata huduma ya uzazi wa mpango 41, saratani ya shingo ya kizazi 23 wamepima na 2 wameonakana kuwa na tatizo hilo” alisema Dkt Mahava.
Madaktari bingwa wanaohudumia katika Huduma hii ya Kliniki Tembezi wanatoka Hospitali ya Benjamini Mkapa, Madaktari kutoka Jiji la Dodoma, Hospitali ya UDOM, Marie Stopes, Engender Health, PSI, UMATI na Egpaf.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweka mkakati wa kupita katika vituo vyake vyote vya Afya kupelekea huduma za kibingwa kupitia Kliniki Tembezi kwa kuanza na Kituo cha Afya Kikombo kinachohudumia watu 12,800 kikiwa na miundombinu ya kutosha.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Patrobas Katambi akipata maelezo kutoka kwa Daktari kuhusu huduma inayoendelea ya Kliniki Tembezi inayoendeshwa na Idara ya Afya ya Jiji ya Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Patrobas Katambi (wa pili kutoka kulia waliokaa), Diwani wa Kata ya Kikombo Mhe. Yona Kusaja (wa kwanza kulia waliokaa), Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt Gatete Mahava (wa tatu kutoka kulia waliokaa) na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa huduma za Klinini Tembezi katika Kituo cha Afya Kikombo.
Baadhi ya wananchi waliofika kufanyiwa uchunguzi wa afya zao wakati wa Uzinduzi wa Huduma za Kliniki Tembezi katika Kituo cha Afya Kikombo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.