MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Dodoma (DUWASA) imesema katika kuhakikisha kuwa huduma ya maji inaboreshwa na kuwafikia watu wote jijini humo, inachimba visima kumi katika maeneo mbalimbali ya jiji lengo likiwa ni kukabiliana na kasi ya ongezeko kubwa la watu inayopelekea mahitaji makubwa ya huduma ya maji.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa kitendo cha Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Sebastian Warioba wakati akizungumza na Mtandao wa Dodoma News Blog Ofisini kwake kuhusiana na Mikakati waliyoipaganga ya kuboresha huduma ya Maji katika jiji la Dodoma.
"Mpaka sasa ninavyozungumza kuna visima kumi vinavyochimbwa, tulianza kuchimba Zuzu na sasa tunachimba eneo la Ihumwa ambapo tumefanikiwa sana, tumepata visima vyenye maji ili tuweze kuhudumia eneo lile na katika eneo la Ntyuka tunataka kufanya vivyo hivyo lakini kwa upande wa Ihumwa tunataka tukichimba tunaweka na pampu na mabomba ili maji yaende kwenye tanki ambalo liko Njedengwa kwenye ukanda wa uwekezaji’’ alisema Warioba.
Wakati huo huo Warioba alisema kuwa, visima vingine kumi vitachimbwa kwenye maeneo mbalimbali katikati ya mji lengo likiwa ni kuongeza kiasi cha maji kwenye mitandao ili wanapotoa maji kwenye chanzo cha Mzakwe yawe yanakuta maeneo hayo ya mtandao yana maji.
"Zaidi ya hapo tumeshirikiana na wenzetu wa mabonde wa Wizara ya Maji na tumeainisha visima vya miaka ya nyuma kama utakumbuka juzi tulikuwa na ziara ya Naibu katibu Mkuu wa Wizara hiyo tulitembelea moja ya visima kama hivyo kiko pale Nzuguni...visima vile vilichimbwa miaka ya nyuma na mpaka sasa tunapozungumza tumeshaainisha visima kumi na tatu vilivyochimbwa miaka hiyo na Serikali, wakati huo kulikuwa na shida ya maji katika mji wa Dodoma lakini baada ya kupata maji ya kutosha visima vile vilikuwa havitumiki kwahiyo tunachokifanya sasa tumevitambau na tumeanza na kile cha Nzuguni na vingine tumeweka wataalamu ambao wanavisafisha kwa maana ya kukarabati na kupima kiasi cha maji yanayotoka mle na ubora wake halafu baadaye tunafunga pampu’’ alifafanua Warioba.
Aliongeza kuwa, Mamlaka hiyo pia imeanzisha magrupu ya mtandao wa kijamii wa 'Whatsapp' kwa ajili ya kupata taarifa mapema ambazo zimekuwa zikijitokeza kwenye maeneo mbalimbali.
"Tuna magrupu kama matatu, magrupu ya 'whatsapp' yapo mawili na moja la 'Telegaram' ambapo tuna watu wengi wamejiunga, lengo letu ni kurahisisha utaratibu wa mawasiliano kati yetu sisi DUWASA na wadau na mwitiko ni mkubwa na tumekuwa tukitoa taarifa mbalimbali kupitia magrupu hayo" aliongeza.
Hata hivyo, alitoa wito kwa wale ambao wamekuwa wakitumia maji kinyume na sheria kuacha mara moja na kwa atakayebainika kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.