Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa taarifa ya ongezeko la wagonjwa wawili wa ugonjwa wa Corona nchini mmoja akiwa ni raia wa Marekani na mwingine ni raia wa Ujerumani na kufanya jumla ya wagonjwa kufikia watatu kutoka mmoja wa awali aliyegunduliwa ambaye ni raia wa Tanzania .
Akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam leo Machi18.2020, Waziri Mkuu amesema wagonjwa hao walioongezeka ni kutoka Dar es Salaan na Zanzibar baada ya sampuli zao kupimwa na kubainika kuwa wana maambukizi ya Virusi vya Corona.
“Tayari wagonjwa wawili wamebainika kuwa na virusi hivyo mgonjwa mmoja kutoka Zanzibar ambaye sampuli zake zimeletwa katika maabara yetu kuu yeye ni mjerumani wa miaka 24 amebainika na virusi hivyo, lakini pia hapa Dar es Salaam kuna mmarekani mwenye miaka 61 naye pia amebainika kuwa na virusi vya Corona “ amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu pia ametangaza kufungwa kwa Vyuo Vikuu na Vyuo vya kati nchini kwa muda wa siku 30 ili kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa wa corona na amemuagiza Waziri wa elimu, kufanya mabadiliko ya mihula ili kutokuleta mkanganyiko kwa wanafunzi hao.
"...sasa leo tunaendelea kuviongeza vyuo vya elimu ya kati na vyuo vikuu vyote nchini, navyo pia tunasitisha kuendelea na masomo, tunatambua vyuo vikuu wanafunzi wengi wako likizo, na sasa tunawataka wasirudi kwenye vyuo vyao na wale wachache waliokuwa wamebaki kwa mitihani nao waondoke mara moja kwenye vyuo hivyo ili kuondoa misongamano kwenye maeneo hayo ya vyuo"; amesema Majaliwa.
Hata hivyo ameasa kuwa, “Tusiwe na taharuki ili tuendelee na shughuli zetu, hatua zitaendelea kuchukuliwa, tupunguze mikusanyiko, maduka na masoko shughuli zitaendelea, huduma za usafirishaji zitaendelea ila abiria wasijazwe, tunawahifadhi wagonjwa tatizo likiisha tutawatoa, Majaliwa ameongeza kuwa;
“Bado tunaendelea kuwa makini kwenye mipaka yetu, tunaendelea kuwa makini kwenye kukagua uingiaji wa wageni ili kujiridhisha kama wote wanaoingia nchini hawana maambukizi,” amesema Majaliwa
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.