IDARA ya Ardhi, Mipango miji na Maliasili katika Jiji la Dodoma itahamia eneo la Micheze lililopo Kata ya Mkonze kwa siku 14 kusikiliza na kutatua kero za wananchi zinazohusu ardhi kwa lengo la kuwasogezea huduma na kuwaharakishia maendeleo wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akiongea na wananchi wa eneo la Michese lililopo Kata ya Mkonze kwenye mkutano wa hadhara jijini hapa jana.
Mafuru alisema kuwa aliamua kwenda kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Michese kutokana na kupokea barua nyingi zinazolalamikia upimaji na changamoto zake. “Maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli ni kwamba viongozi tutoke ofisini na kuwafuata wananchi kuwasilikiza na kutatua kero zao. Nikiwa ofisini nimekuwa nikipokea barua nyingi kutoka Kata ya Mkonze, zikilalamikia juu ya upimaji na changamoto zake. Sasa kama kiongozi, wingi wa barua hizo za malalamiko unanipa picha kuwa kuna tatizo, ndiyo maana nimekuja hapa na timu yangu kuwasikiliza na kutatua changamoto hizo” alisema Mafuru.
Katika masaa yake matano ya kupokea, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, mkurugenzi huyo aliiagiza Idara ya Ardhi, Mipango miji na Maliasili katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenda na kuweka kambi katika eneo la Michese kusikiliza changamoto ya kila mwananchi na kuitatua. “Ndugu zangu, nitagawa timu ya wataalam wangu wa jiji, kampuni ya upimaji, timu ya urasimishaji na viongozi wa mitaa katika mitaa mitatu ya eneo la michese kuanzia Jumatatu. Watakaa hapa kwa siku 14 kupokea na kusikiliza kila mwananchi lalamiko lake na kulipatia ufumbuzi. Malalamiko yatakayohitaji kwenda ‘site’ wataenda” alisema Mafuru.
Aidha, aliitaka kampuni inayofanya zoezi la upimaji kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kwa uwazi ili kuwatendea haki wananchi. “Naiagiza kampuni inayofanya zoezi la upimaji kubandika ramani zote za utambuzi katika mbao za matangazo kwenye ofisi za mitaa yote zoezi lilipotekelezwa ili kila mwananchi aone na kumtambua jirani yake. Vilevile, bandikeni ramani za Mipango miji. Ramani hizi zikibandikwa na maelezo yake kutolewa kwa uwazi zitaondoa lugha ya ubabaishaji na kuonesha uwajibikaji na hatimae kuondoa malalamiko” alisisitiza Mkurugenzi Mafuru.
Kwa upande wake, mkuu wa Idara ya Ardhi, Mipango miji na Maliasili, Amelye Chaula alisema kuwa hakuna kiwanja kitakachouzwa kinyemela katika eneo hilo. “Ndugu zangu, niwatoe hofu, hivi viwanja baada ya kukamilika ramani ndio zoezi la ugawaji litaanza rasmi. Mmemsikia Mkurugenzi wa Jiji maelekezo aliyotoa, lazima ramani zote zibandikwe na kila hatua ifanyike kwa uwazi. Hivyo, kama kuna aina yoyote ya ugawaji ambayo imefanyika, imefutwa rasmi” alisema Chaula.
Naye Afisa Mipango miji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aisha Masanja alisema kuwa zoezi la upimaji shirikishi linalofanyika katika eneo la Michese linalenga kuboresha eneo hilo ili liwe linajitosheleza kihuduma. “Halmashauri tunataka kuwa na Michese inayojitosheleza kwa kuwa na huduma zote muhimu ili kuwaondolea kero wananchi kufuata huduma maeneo ya mbali. Tumesikia malalamiko ya wananchi juu ya umilikishaji ardhi. Napenda kuwahakikishia wananchi kuwa zoezi la umilikishaji ardhi litafanywa na halmashauri na siyo kampuni ya upimaji. Halmashauri ndiyo yenye mamkala kisheria kumilikisha ardhi. Hivyo, hakuna ardhi itakayomilikishwa na kampuni ya upimaji” alisema Masanja kwa kujiamini.
Kata ya Mkonze ina jumla ya mitaa nane ambayo ni Chidachi, Miganga, Chinyika, Chisichiri, Muungano A, Muungano B, Bwawani na Nzinje.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.