HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imewataka maafisa watendaji kata kujiamini na kuhakikisha lengo la ukusanyaji wa mapato ya halmashauri linafikiwa ili serikali iweze kutoa huduma bora kwa wananchi wake.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mweka Hazina wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA Rahabu Philip (pichani) alipokuwa akiongea na maafisa watendaji wa kata za jiji hilo katika kikao cha kawaida cha kukumbushana wajibu wa maafisa watendaji wa kata katika kukusanya mapato ya halmashauri.
CPA Philip alisema kuwa maafisa watendaji wa kata wana wajibu wa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya halmashauri katika kata zao. “Maafisa watendaji wa kata ndiyo vidole vya Mkurugenzi wa Jiji, na bahati nzuri vyanzo vyote vya mapato vipo katika kata zenu. Mkurugenzi hana kata ya kukusanya mapato. Ushuru wa huduma unapatikana kwenye kata, ushuru wa hoteli unapatikana kwenye kata, ushuru wa madini ujenzi unapatikana katika kata. Hivyo, mnatakiwa kujiamini katika kutekeleza majukumu yenu” alisema CPA Philip.
Akiongelea uvujaji wa mapato ya halmashauri, alisema kuwa wote wakitimiza wajibu hakuna mapato yatakayovuja. “Hata tunapoongelea uvujaji na upotevu wa mapato ya halmashauri, mtu wa kwanza kufahamu uvujaji huo ni mtendaji wa kata, hivyo wajibu wenu katika kuhakikisha serikali inakusanya mapato yake ni mkubwa sana” alisisitiza CPA Philip.
Kwa upande wake, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Donatila Vedasto aliwakumbusha maafisa watendaji hao kusimamia ukusanyaji wa leseni za biashara. “Ukusanyaji wa leseni za biashara ni jukumu letu sote. Maafisa biashara hatuwezi kufika katika maeneo yote ya halmashauri, ila maafisa watendaji wa kata kwa kushirikiana na maafisa watendaji wa mitaa tunaweza kuyafikia maeneo yote ya biashara” alisema Vedasto.
Aidha, aliwataka kuwatambua wafanyabiashara wote waliopo na wanaoanzisha biashara mpya ili waweze kukata leseni na serikali kupata mapato yake. Alisema kuwa halmashauri imeanzisha utaratibu wa kupata taarifa za kila robo kufahamu idadi ya leseni zilizokatwa, idadi ya leseni zilizoisha muda wake na idadi ya leseni zilizohuishwa kutoka katika kata.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina kata 41 na jumla ya mitaa 222.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.