MAMLAKA za Serikali za Mitaa nchini zimetakiwa kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujenga majengo ya vitega uchumi ili ziweze kujitegemea.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa Jumuiya ya Serikali za mitaa (ALAT) kwa niaba ya Rais Dkt John Magufuli jijini Mwanza jana.
Majaliwa alisema kuwa Mamlaka za Serikali za mitaa zinakusanya fedha lakini haziendi kwenye miradi ya maendeleo. Hivyo, alizitaka kutenga asilimia 40 ya mapato yake kwa ajili ya shughuli za maendeleo. “Kuna Halmashauri nyingi zinafanya vizuri kwenye makusanyo lakini fedha hazijulikani zinaenda wapi, Dare s Salaam, Arusha ni baadhi ya zinazokusanya fedha lakini hamna mradi hata mmoja. Ukichukulia Dar es Salaam au Arusha ambao wanakusanya kati ya shilingi Bilioni tano na 10, ni mradi gani wa thamani kubwa uliojengwa kwa kutumia fedha zenu za ndani, ukiacha hii mikubwa ya stendi ya mabasi au barabara za lami ambayo inajengwa kwa fedha za serikali kuu?” alihoji Majaliwa.
Alizitaka Halmashauri hizo kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inayojenga majengo ya biashara kwa mapato ya ndani. “Afadhali hawa wa Dodoma ambao wanajenga stendi ya mabasi na hoteli mbili za kitega uchumi” alisema Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa.
Aidha, alizitaka Halmashauri kujenga miradi mikubwa inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Hasa ikizingatiwa kuwa Halmashauri zina jukumu kubwa la kutoa huduma za kwa wananchi walio katika maeneo yao ya kiutawala.
Mkutano wa ALAT unafanyika jijini Mwanza kwa siku tatu ukihudhuriwa na washiriki zaidi ya 600 wakiwemo Mameya wa Majiji na Manispaa, Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za mitaa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.