Uzinduzi rasmi wa Ikulu yetu ni tukio kubwa la historia kwa Taifa letu. Tuungane sote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufikia hatua hii adimu na adhimu, miaka 50 toka Serikali ilipoweka azimio la kuhamisha Makao Makuu ya Nchi kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma.
Ikulu hii ni kilele katika azma ya Serikali kuhamia Dodoma. Safari ya miaka 50 kufikia siku hii ni ya demokrasia kwani nia ya kuhamia Dodoma ilipitishwa na Halmashauri Kuu ya TANU mwaka 1973, baada ya kura ya maoni katika matawi yake nchi nzima. Safari hii ina mchango wa namna yake kwa kila awamu iliyowahi kuiongoza nchi yetu:
1. Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
2. Alhaji Ali Hassan Mwinyi
3. Hayati Benjamin William Mkapa
4. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
5. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli
Ikulu ni ya kila Mtanzania na kupitia sanduku la kura sote tunaamua nani wataingia katika kipindi fulani kutumikia Watanzania wote. Ujenzi wa Ikulu yetu wenyewe kwa nguvu zetu, fedha zetu na utaalamu wetu ni moja ya shuhuda za uhuru wetu kama nchi.
Mzee wetu Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema, “Maisha ni hadithi", tuandike hadithi njema za maisha yetu. Julai 25, 2016 Hayati Rais Magufuli aliukumbusha Mkutano Mkuu wa CCM kuhusu uamuzi wa kuhamia Dodoma na chini ya Awamu yake ujenzi huu ambao tumeukamilisha ulianza rasmi. Hayati Rais Magufuli ameandika hadithi yake.
SOURCE- Instagram: Samia_Suluhu_Hassan
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.