SHIRIKA la Kazi Duniani (ILO) limeipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu ili kuwezesha shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
ILO limesema kutokana na ufanisi huo, lipo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa na kwamba, linaamini miradi hiyo mikubwa itasaidia kuongeza ajira kwa wananchi.
Mratibu wa Programu ya Kitaifa ya ILO, Mpango wa Uwekezaji wa Kina Jamii na Uajiri (EIIP), Dampu Ndenzaro, alisema hali hiyo itasaidia pia kuwapa nafuu hata watu walio pembezoni kutokana na msimamo wa serikali wa kutaka miradi hiyo kutekelezwa na wafanyakazi wazawa kwa kutumia malighafi za ndani.
Alikuwa akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya teknolojia ya ujenzi yaliyofanyika Chamwino mkoani Dodoma aliposisitiza kuwa, ILO linafurahishwa na mikakati ya serikali.
Mafunzo hayo ya Agosti 17 hadi Septemba 4, 2020 yaliendeshwa na Taasisi ya Mafunzo ya Teknolojia (ATTI) yenye makao makuu Mbeya kwa ufadhili wa ILO yakikutanisha washiriki 20 wakiwemo wa ATTI yenyewe, TARURA, TANROADS, TASAF na Zanzibar.
Washiriki wengine walitoka Bodi ya Mfuko wa Barabara, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi ya Mafunzo ya Ujenzi ya Morogoro, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu pamoja na wakandarasi wanne wa kazi kutoka Lindi, Mbeya, Rukwa na Dodoma.
Miongoni mwa miradi iliyoifurahisha ILO ni ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki, ujenzi reli ya kisasa (SGR) na mradi wa umeme kwenye Bwawa la Julius Nyerere.
Akizungumzia mafunzo hayo, Ndenzaro alisema yalilenga kujifunza teknolojia mpya na kuonesha utumiaji wa teknolojia zinazowezekana kwa shughuli ukiwemo ujenzi wa barabara.
Alisema, wakati wa kuongoza mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elius Mwakalinga, aliishukuru ILO, kwa kuwa tayari kushirikiana na serikali kutoa mafunzo kwa manufaa ya taifa.
Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Teknolojia (ATTI), Mahmoud Chamle, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhimiza matumizi ya teknolojia ya gharama nafuu katika miradi.
Source: HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.