BALOZI wa Indonesia nchini Tanzania Bw. Tri Yogo Jatmiko pamoja na ujumbe wake, wamemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ofisini kwake leo Septemba 19 kuzungumza kuhusu utaratibu wa kuhamishia ofisi za Ubalozi huo kwenye Mji Mkuu wa Serikali Dodoma kwa lengo la kutekeleza agizo la Serikali la kuhamishia Makao Makuu ya nchi Mkoani Dodoma na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika mazungumzo yao Balozi Jatmiko amesema mwezi uliopita Rais wa Indonesia alikuja Tanzania na kuonana na Mhe. Rais Samia ambapo moja ya mambo waliyozungumza lilikua ni swali kutoka kwa Mhe. Rais Samia kuhusu lini Ubalozi wao utahamia Dodoma. Kufuatia mazungumzo ya viongozi hao, Mhe. Balozi ameamua kufunga safari hadi kwenye ofisi hii ili kupata utaratibu wa ujenzi wa ofisi za Ubalozi kutoka kwa mwenyeji wao Mhe. Senyamule.
Akitoa ufafanuzi juu ya eneo lililotengwa kwa ajili ya Mabalozi wa nchi mbalimbali katika Mji wa Serikali Mtumba, Mratibu wa Mradi wa ujenzi wa Mji wa Serikali Dodoma Bw. Meshack Bandawe, amesema kuwa Balozi zote zilizopo nchini zimetengewa maeneo maalumu na yenye ukubwa unaolingana wa heka 2.5 kwa eneo la ofisi na pia kuna maeneo kwa ajili ya makazi na watumishi wa Balozi hizo. Amewaonyesha ramani ya eneo lao ikiwemo majirani waliopakana nao ambao ni Ubalozi wa Burundi, Algeria, Namibia pamoja na Vietnam. Hata hivyo, amebainisha kuwa ujenzi wa Mji wa Serikali kwa sasa umefikia asilimia 70 hadi 80.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Senyamule, ameupongeza Ubalozi huo kwa kufuatia taratibu za ujenzi wa ofisi za Ubalozi na kuhamia Dodoma kwakuwa ni wakati sahihi kwao kulingana na miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kujengwa Dodoma ikiwemo uwanja wa ndege wa Msalato ambao utarahisisha shughuli za safari za kuingia na kutoka Dodoma. Pia amezungumzia ujenzi reli ya kisasa ya SGR ni miradi mingine ya kimkakati itakayorahisisha shughuli za kibalozi zitakapokua ndani ya Mkoa wa Dodoma.
Balozi Jitmiko amesisitiza kupatiwa nyaraka zitakazohusiana na eneo lao ili aweze kuziwasilisha kwa Waziri wao na kujadiliwa kwenye Bunge la Indonesia kwa ajili ya kupangwa bajeti ya ujenzi ili uweze kuanza mara moja. Pia Balozi huyo amesema Indonesia ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya kiteknolojia ikiwemo kwenye sekta za madini na umeme kwani huko kwao wana teknolojia za kisasa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (kulia) akimkaribisha mgeni wake Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Bwana Tri Yogo Jatmiko ofisini kwake jengo la Mkapa jijini Dodoma leo.
Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Bwana Tri Yogo Jatmiko (wa kwanza kulia) akiwa ameambatana na ujumbe wake akiweka saini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Mratibu wa Mradi wa Ujenzi wa Mji wa Serikali Dodoma Bwana Meshack Bandawe (aliyesimama) akiwaonesha Balozi wa Indonesia nchini na ujumbe wake ramani ya eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Mabalozi kwenye Mji wa Serikali Mtumba.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.