Serikali imeziagiza halmashauri zote nchini kukarabati samani za shule kupitia fedha zinazopelekwa shuleni za program ya Elimu Bila Malipo ili kuondoa tatizo la madawati kwenye shule nchini.
Kauli hiyo iliitoa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo tarehe 20/02/20202 wakati akipokea taarifa ya tafiti iliyofanya kati ya Chuo Kikuu cha Dodoma na taasisi ya Mdigri Logistics kuhusu vifaa vya Ufundishaji na Ujifunzaji kwenye shule za sekondari. Tafiti hiyo imefanyika katika mkoa wa Dodoma na hafla ya kukabidhi taarifa ilifanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.
“nielekeze Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Halmashauri zote kwa Wakurugenzi, kupitia na kushughulikia madawati na meza zote na kuhakikisha zinakarabatiwa kupitia fedha za Elimu Bila Malipo”
Jafo amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia vikundi vya vijana kufanya ukarabati wa miundombinu ya madarasa, madawati na vifaa vingine vya shule ikiwa ni sehemu ya kuwapa ajira vijana na kuboresha mazingira ya elimu katika shule zilizopo kwenye mamlaka zao badala ya kusubiri kutenga fedha kutengeneza madawati mapya.
“Halmashauri zitumie vikundi vya vijana kufanya uakarabati wa miundombinu ya madarasa, madawati na vifaa vilivyopo katika shule, haiwezekani kusubiri kutenga fedha za madawati mapya wakati yapo madawati ya zamani na hayajakarabatiwa” alisema Waziri Jafo.
Vilevile, Waziri Jafo amesema pamoja na watendaji hao kukarabati samani za shule pia wakarabati miundombinu ya shule yakiwemo majengo, matundu ya vyoo, madarasa na miundombinu mingine kwenye sekta ya elimu iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.
Aidha amewataka Wakuu wa shule kuendelea kusimamia masuala ya kitaaluma, mazingira na miundombinu kama kipaumbele chao na kuboresha hali ya taaluma nchini.
Jafo amewataka watafiti hao na wengine kuendelea kufanya tafiti kwenye sekta ya elimu na kuyapa kipaumbele maeneo mengine kama miundombinu ya vyoo, madarasa na vinakilishi ili kutoa mchango wa kufanya maboresho kwenye elimu ya msingi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Satano Mahenge amesema watafiti wamefanya tafiti na kubaini tunalo tatizo katika eneo la elimu na kwamba watanzania hatuna utamaduni wa kukarabati madawati na miundombinu hivyo tafiti itatusaidia kuboresha miundombinu kwenye sekta ya elimu.
Awali Dkt. Ombeni Msuya kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma aliwasilisha taarifa ya tafiti ya vifaa vya Ufundishaji na Ujifunzaji kwenye shule za sekondari 35 na kusema kuwa utafiti huo umefanyika kwenye Halmashauri 7 zote za mkoa wa Dodoma kuanzia mwezi Januari, 2019 hadi januari, 2020 na kubaini changamoto kadhaa ikiwemo kutokuwepo kwa zana za kufundishia zinazokidhi mahitaji, kuwepo kwa viti, meza na vifaa vya maabara visivyo na ubora, kuwepo kwa meza 91,000 na viti 915 ambavyo havitumiki na vinahitaji ukarabati mdogo.
Dkt. Msuya ametoa rai kwa Serikali kuundwa kwa kikundi kazi kitakachokuwa kinakarabati samani na miundombinu ya shule ‘Maintainance Mobile Unit’ ambao wanaweza kutoka katika vyuo vya ufundi ili kuendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia shuleni.
Kwa upande wake Yoram Mkwawa Mkuu wa shule Mbabala ametoa rai ya kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu Sera ya Elimu Bila Malipo kwani kuna upotoshwaji mkubwa kuhusu sera hiyo ambapo wazazi wengine hawapo tayari kuchangia chochote kwa ajili ya maendeleo ya shule zao lakini pia amewataka Wakuu wa shule kuwa wabunifu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali shuleni badala ya kusubiri fedha kutoka Serikalini.
Chanzo: Tovuti ya tamisemi.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.