Serikali imetoa wito kwa watanzania kutunza miundombinu mbali mbali iliyowekezwa na Serikali nchini ili kuendelea kuwekeza fedha katika maeneo mengine na kupangua wigo wa maendeleo nchini.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (pichani juu) wakati wa akitoa mrejesho wa mafanikio yaliopatikana katika sekta ya miundombinu katika kipindi cha miaka mitano 2015 – 2020 leo Jijini Dodoma katika Siku ya TAMISEMI (Miundombinu).
Aidha Mhe. Jafo amesema kuwa ni wajibu wa kila mtanzania kulinda miundombinu hiyo kwa kutoa ushirikiano kwa serikali pale ambapo wanaona kuna watu ambao wanakwenda kinyume na taratibu za utumiaji wa miundombinu iliopo katika maeneo yao.
“wale wanaong’oa taa za barabarani, alama za barabarani, wanaozidisha kipimo cha ubebaji mizigo kwenye barabara zilizojengwa mijini na vijijini hao sio watu wema kwa nchi yetu, kwani wanarudisha maendeleo ya Taifa letu nyuma”, amefafanua Mhe. Jafo.
Waziri Jafo amesema kuwa watanzania wafahamu kuwa sekta ya miundombinu nchini imesaidia Watanzania kuinua uchumi wao na kuchangia taifa kufikia uchumi wa kati kwani wananchi sasa wanasafirisha mazao yao bila changamoto kama ilivyo kuwa hapo awali.
“Neema hiyo ni kutokana na maono ya Rais Magufuli aliyetoa kiasi cha shilingi Ttririoni 3.6 kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbali mbali ili wananchi wapate huduma za kijamii bila vikwazo hususani, mtandao wa barabara za mijini na vijijini”, amebainisha Mhe.Jafo.
Lakini pia Mhe. Jafo amesema kupitia sekta hii zaidi ya vituo vya mabasi 24 vya kisasa vimejengwa katika maeneo mbali mbali nchini kwa lengo la kuwapatia Watanzania huduma sahihi kutokana na kodi zao.
Mhe. Jafo ameongeza kuwa sehemu za kupumzikia nane nchini zimejengwa kisasa ili pale mwananchi akiwa amechoka kutoka katika majukumu yake anapitia pale kupumzika na akili yake kuwa sawa na kuendelea na majukum yake ya utafutaji.
Katika hatua nyingine Mhe. Jafo ameeleza majukumu makubwa na mafanikio ya sekta ya miundombinu chini ya TAMISEMI kuwa ni ujenzi wa machinjio ya kisasa, ofisi mpya za wakuu wa wilaya, nyumba za wakuu wa wilaya na ujenzi wa masoko ya kisasa nchini.
Vilevile, Mhe. Jafo ametoa shukurani za dhati kwa watendaji wake wote kwa ushirikiano waliompatia katika kufanikisha hayo, TAMISEMI inajibu matatizo ya Watanzania kwa kuwasogezea huduma za kijamii katika ngazi za msingi na kutatua kero zao kwa wakati ili kusukuma maendeleo kwa ujumla.
Naye Naibu Waziri TAMISEMI, Josephat Kandege amesema kuwa matunda ya mafanikio yote yanayoshuhudiwa na Watanzania ni kutokana na ushirikiano mzuri wa watendaji waliokuwa wakionyesha katika kutoa huduma kwa watanzania.
“Mafaniko huletwa na ushirikiano mzuri baina ya watendaji hivyo matokeo yake ni kupata malengo chanya ya kuleta maendeleo kwa wananchi waliompa dhamana Rais Magufuli na yeye kuamua kuona tunafaha kuwa wasaidizi wake katika kuwatumikia Watanzania”, amesisitiza Mhe. Kandege.
Naibu Waziri TAMISEMI, Mhe. Josephat Kandege akizungumza na Watanzania wakati wa hafla ya kutoa mrejesho wa mafanikio ya sekta ya miundombinu ndani ya miaka mitano (2015 - 2020).
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (wa tatu kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Afya TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe (wa pili kushoto) wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa mafanikio yaliyofanyika ndani ya miaka mitano chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI leo Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (wa tatu kushoto) akipatiwa maelekezo na mtaalamu wa sekta ya miundombin juu ya kilichofanyika ndani ya miaka mitano
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.