SERIKALI imefanya mabadiliko katika muundo wa kanuni za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ambapo kwa sasa katika kundi la vijana na wamama kikundi kinaweza kupokea mkopo kuanzia watu watano na kwa walemavu hata mtu mmoja anaweza kupokea mkopo.
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa mwaka wa chama cha wataalamu wa Maendeleo ya Jamii uliofanyika kwa siku tatu jijini Dodoma.
Amesema alipokea maombi mengi kuhusu kanuni inayotaka kikundi lazima kuwa na watu kuanzia kumi kuwa baadhi ya maeneo imekuwa changamoto kuwapata watu wanaokubaliana na kuwa Pamoja na kutembea Pamoja.
“Katika maeneo mengi ni vigumu sana kuwapata watu wanaokubaliana kuwa Pamoja hadi kufikia kumi, na hasa kwa walemavu imekuwa ngumu kuwapata kumi wenye ulemavu wa aina moja, sasa hata mtu mmoja mwenye ulemavu anaweza kukopa” amesema Mhe. Jafo.
Amesema kuanzia sasa maafisa maendeleo ya jamii watapata nakala za kanuni mpya zitakazo kwenda kuwaongoza katika kutekeleza majukumu yao katika maeneo yao ya kazi kundi la vijana na kundi la akina mama hata wakikubaliana wakifikia watano wataruhusiwa kupata mikopo hiyo.
Aidha amebainisha kuwa wamefanya marekebisho hata katika kuhakikisha urejeshwaji wa mikopo hiyo unaimarika sasa watatenga fedha kwa ajili ya ufuatiliaji wa mikopo, halmashauri zimetengwa katika makundi ambapo halmashauri zenye mapato yasiyozidi bilioni moja lazima watenge kila mwezi kiasi cha laki tano hadi milioni moja.
Wakati katika halmashauri zenye mapato kuanzia bilioni 1 hadi bilioni 2 wao watatenga kiasi cha shilingi milioni moja hadi milioni moja na nusu, na kwa halmashauri zinazokusanya kuanzia bilioni 5 na kuendelea lazima watenge kiasi cha shilingi milioni 5 kila mwezi kwa ajili ya kuwawezesha maafisa maendeleo ya jamii kuvifuatilia hivyo vikundi.
“Nasisitiza fedha hizi ni kwa ajili ya marejesho ya mikopo na sio fedha zilizotengwa kwahiyo kama hufuatilii vikundi hivyo au hakuna marejesho ya vikundi fedha hizi zisitengwe, tunafanya hivi ili ufuatiliaji uimarishwe” amesema.
Amesema kwa miezi sita tayari serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 24, na kwa kipindi cha miaka mitano serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 143 kutoa kwa vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu kote nchini.
Amewashukuru wataalamu wa maendeleo ya jamii kwa kazi kubwa wanayoendelea kufanya hapa nchini na kubainisha kuwa kwa sasa kitengo hicho kinazidi kuimarika tofauti na hapo mwanzo ambapo kilikuwa kikidharaulika sana.
Amesema katika maeneo yao ya kazi kuna miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii umuhimu wa miradi hiyo na itakavyowanufaisha wananchi wenyewe ili wailinde kikamilifu.
Amewataka kutumia mafunzo waliyoyapata kupitia mkutano huo kwenda kufanya kazi kwa ufanisi ukubwa ili taifa kupata tija kwa sababu wao ndio kiungo muhimu katika maendeleo ya yananchi katika maeneo hayo hivyo wahamasishe wananchi katika kujipatia maendeleo yao.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amesema wataalamu hao wamekutana kwa siku tatu kwa lengo la kujadili namna ya kuboresha taalamu hiyo katika maeneo yao ya kazi.
Amesema kwa sasa wameboresha mkutano huo, kwani awali walikuwa wakihudhuria wakuu wa idara pekee lakini kwa sasa wanashirikisha wataalaumu wote hadi ngazi za chini kabisa ili kuboresha taaluma, na kwa mwaka huu wamewakutanisha na watunga sera ili elimu hiyo iwefikie kwani wao ndio watekelezaji wa sera hiyo.
Katika mkutano huo umetumika katika kuchagua viongozi wapya watakaoongoza wataalamu wa chama kwa kipindi kingine ambapo nafasi ya mwenyekiti ameshinda Bi Angela Mvaa, Makamu mwenyekiti Dkt Regina Malima na kiti cha katibu Mkuu ni Daniel Wambura.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.