Na. Faraja Mbise, DODOMA
Jamii imeaswa kutoyafumbia macho masuala ya ukatili wa kijinsia na kutakiwa kuripoti kwenye vyombo vya sheria matukio ya ubakaji, ulawiti na ndoa za utotoni.
Hayo, yalisemwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ng’hongh’onha, Patrick Mwachambi ambaye ni muwakilishi wa mgeni rasmi, alipokuwa akizungumza na wananchi waliojitokeza katika Uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ngazi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Kata ya Ng’hong’onha.“Natoa wito kwa wananchi wenzangu, kuwatumia ipasavyo wataalam wetu kwasababu wako tayari wakati wote kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili vinakomeshwa na wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria. Namshukuru sana Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, tumejifunza mengi kupitia wataalam. Kwahiyo, nawaomba wananchi tuzingatie elimu tuliyopewa na kuahidi kuifanyia kazi, yote yaliyoelekezwa tutayatekeleza bila kuathiri taratibu za kisheria” alisisitiza Mwachambi.
Akizungumzia kampeni ya mwaka huu isemayo “Kuelekea miaka 30 ya Beijing: CHAGUA Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia” mgeni rasmi alitoa historia fupi kuhusiana na harakati za kupambana na kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
“Kaulimbiu hii inaendelea kusisitiza kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili yaliyoanza miaka mingi nyuma na kutiliwa mkazo na Mkutano wa Beijing wa mwaka 1995 ambao ni mkutuno wanne wa Dunia kwa wanawake uliofanyika Beijing nchini China. Mkutano huu uliwakutanisha kwa pamoja serikali za mataifa mbalimbali pamoja na wanaharakati, na uliwezesha kuundwa kwa jukwaa la kuchukua hatua la Beijing, na agenda ya msingi ya haki za wanawake katika ngazi za kimataifa ambao kati ya malengo yake makubwa ni kutokomeza ukatili wa kijinsia na kusisitiza upatikanaji wa haki za wanawake katika nyanja zote za kimataifa na kutetea haki za kijinsia” alisema Mwachambi.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii ambae ni Mratibu wa Jinsia na Watoto Jiji la Dodoma, Fatuma Daudi, alizungumzia mlolongo wa matukio mbalimbali ambayo yanaadhimishwa ndani ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia. Daudi alisema “tukiwa tupo katika kampeni za siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, kampeni hizi zinatokana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Kimataifa Kofi Annan ambaye aliona vitendo vya ukatili wa kijinsia unazidi hivyo kitengwe kipindi maalum cha kufanya kampeni ili kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia. Kipindi kilichaguliwa kuanza tarehe 25 Novemba na kuisha tarehe10 ya mwezi Desemba, ukizihesabu siku hizi zinafika siku 16, ndani ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kuna siku mbalimbali zenye matukio maalum kati ya hizo kuna siku ya Novemba 25, ambayo ni siku ya kupinga ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake, Novemba 29, ambayo ni siku ya kimataifa ya utetezi wa haki za wanawake, Desemba moja ambayo ni siku ya UKIMWI Duniani, Desemba 05, siku ya kujitolea Duniani na siku hizi zinahitimishwa na tarehe 10 Desemba, ambayo ni siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Siku hizi zote zipo ili kuhakikisha wanawake, watoto na Jamii kwa ujumla inaepukana na vitendo vya ukatili”.
Kuhusu msaada wa kisheria unaopatiwa kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, Afisa Maendeleo ya Jamii, Dawati la Msaada wa Kisheria katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Frida Ngowi aliogelea umuhimu wa dawati la sheria katika kupambana na masuala ya ukatili wa kijinsia.
“Dawati hili la msaada wa kisheria lipo kwa ajili ya kutoa elimu ili watu tufahamu haki zetu, pili dawati hili linawasaidia watu kupata huduma za msaada wa kisheria ambapo kuna makundi maalumu, kundi la kwanza ni wanawake, watoto, walemavu na wazee lakini pia mwananchi yeyote ambaye hana uwezo wa kumudu gharama za mahakama. Kwahiyo, huduma tunazotoa ni pamoja na ukatili wa kijinsia unaotendeka kwa wanawake, watoto na wanaume pia wanaopitia changamoto za ukatili wa kijinsia” alisisitiza Ngowi.
Vilevile, Afisa Ustawi wa Jamii Mwanadamizi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aneth Mwambya aliwasisitiza watoto kutoa taarifa kwa wazazi, dawati la kijinsia au kwa walimu endapo watakutana na vitendo hivyo viovu vya ukatili wa kijinsia. “Ukatili wa ngono au kingoni, tunauona, tunaenda likizo, takwimu zinasema asilimia 60 ya ukatili unafanyika nyumbani, unapofanyiwa kitendo chochote ambacho si kwa ridhaa yako kwa maana unapata madhara kiakili, kimwili na kingono unatakiwa utoe taarifa kwa wazazi, jirani kama unamwamini, dawati la jinsia, kituo cha polisi na serikali za mitaa” alisisitiza Mwambya.
Nae Mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Ng’hong’onha, Theresia Samson alitoa rai kwa watoto wanaopitia ukatili wa kijinsia majumbani kwao, waweze kuripoti matukio hayo ili kupunguza idadi ya matukio ya ukatili wa kijinsia. “Mimi nimeigiza kama mtoto niliyebakwa na mjomba, nawashauri watoto wengine wanaofanyiwa vitendo hivi wasikae kimya wakatoe taarifa kwa walimu, watu wanaowaamini au kwa wazazi wao” alishauri Samson.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.