JAMII imetakiwa kuwa chachu ya mapambano dhidi ya UKIMWI katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kufikia asilimia sifuri ya maambukizi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Emmanuel Chibago alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Jiji la Dodoma waliojitokeza kwa wingi katika maashimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika ngazi ya Wilaya ya Dodoma mjini katika Kata ya Hombolo Bwawani leo.
Chibago amesema “kaulimbiu ya maadhimisho haya ni Jamii ni chachu ya mabadiliko; tuungane kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Kaulimbiu hii inaitaka jamii mzima kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI”. Katika ushiriki huo wa jamii, jamii inatakiwa kuvunja ukimya na kupaza sauti, aliongeza. “Jambo la muhimu hapa ni kuvunja ukimya katika kupambana na maambukizi mapya katika jamii” alisema Chibago. Kiwango cha maambukizi katika Mkoa wa Dodoma ni asilimia 5.1, ambacho alikitaja kuwa bado kipo juu.
Naibu Meya huyo ambape pia ni Mwenyekiti wa kamati ya kudhibiti UKIMWI katika Halmashauri hiyo, amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi, kutokana na nafasi hiyo ya kimkakati ni wazi kuwa itapokea idadi kubwa ya wageni wa aina tofautitofauti. “Pamoja na neema ya kupokea wageni katika Jiji letu la Dodoma, tutapokea na mambo mengine ambayo yatachochea ongezeko la maambukizi ya virusi vya UKIMWI, lazima tuwe makini na kuchunga tabia zetu na kuepuka ngono zembe” amesisitiza Chibago.
Aidha, amesema kuwa Halmashauri itaendelea kuwasaidia watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo na kuwawezesha kiuchumi. Halmashauri imekuwa ikiwapatia mikopo kupitia vikundi vya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, na kuahidi kuendelea kufanya hivyo ili kuwajengea uchumi imara.
Katika hatua nyingine Naibu Meya ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matumbulu ameviomba vyombo vya dola kutoa ushirikiano na kuharakisha uchunguzi pale mashauri ya ngono yanapowasilishwa ili kuwawezesha wananchi kupata haki kwa wakati na kupunguza ongezeko la maambukizi. Amesema kuwa baadhi ya mashauri yamekuwa yakichelewa na kuwafanya mlalamikaji kuchelewa au kukosa haki zao.
Katika taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kudhibiti UKIMWI kwa kipindi cha mwaka 2018 hadi 2019 iliyosomwa na Mratibu wa kudhibiti UKIMWI Halmashauri ya Jiji la Dodoma Daisy Kanyanga amesema yalifanyika mafunzo ya wajibu na majukumu ya kamati za Kata na Mitaa za kudhibiti UKIMWI kwa lengo la kuimarisha utendaji wake. “Zoezi la ufuatiliaji na usimamizi wa kamati za kudhibiti UKIMWI ngazi ya Kata na Mitaa lilifanyika kwa lengo la kuhakiki utekelezaji wa utendaji na mipango kazi ya kamati, kuhakiki uendeshaji wa vikao vya kamati za kudhibiti UKIMWI kwa Kata na Mitaa ya Jiji la Dodoma” alisema Kanyanga. Aidha, jumla ya kondomu za kiume 140,220 na kondomu za kike 3,000 zilisambazwa sambamba na elimu ya matumizi sahihi ya kondomu hizo katika kupambana na maambukizi mapya, ameongeza.
Naibu Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Emmanuel Chibago akiongea katika maashimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika ngazi ya Wilaya ya Dodoma mjini katika Kata ya Hombolo Bwawani leo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.