WAKAZI wa Jiji la Dodoma wametakiwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa kila makazi na taasisi zote jijini hapa zinakua na huduma ya vyoo bora pamoja na kuweka sehemu maalum za kunawia mikono ili kuikinga jamii dhidi ya maradhi yanayoenezwa kwa njia ya uchafu.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Dkt. Gatete Mahava (aliyesimama pichani juu), katika maadhimisho ya siku ya unawaji mikono Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya soko la Majengo Jijini hapa.
Akimuwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt. Mahava, amesema Jamii inatakiwa kujenga mazoea ya kunawa mikono wakati wote hali inayoweza kuokoa maisha na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwasababu pasipokuwa na afya bora wananchi hawataweza kufanya shuguli za uzalishaji mali hivyo uchumi wa mtu binafsi unashuka na kupelekea hata uchumi wa Taifa kuporomoka pia.
"Unawaji wa Mikono ninaufananisha na kinga ambayo mtu anajikinga mwenyewe, afya bora kupitia usafi wa mikono ni moja ya misingi ya kuitambua jamii kuwa ni waastaarabu na hatuwezi kuwa na afya bora kama hatujawekeza kwenye masuala muhimu ya kulinda afya zetu" Alisema Dkt. Mahava.
Pia alisisitizia Taasisi za Elimu kuhakikisha wanawajengea wanafunzi mazoea ya kupenda usafi wao binafsi na mazingira yanayowazunguka ili kutengeneza kizazi kitakachokuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha jamii inakua safi na salama na kuondokana na magonjwa ya milipuko.
Kwa upande wake Afisa Afya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Abdallah Mahia amewataka wananchi kuyafanyia kazi yale yote waliyoyapa katika siku ya maadhimisho na kulinda miundombinu ya kunawia iliyowekwa katika maeneo mbalimbali Jijini hapa.
Mahia aliongeza kuwa swala la unawaji wa mikono ni endelevu na halikuwepo kwa ajili ya Janga la Corona tu bali hata baada ya janga hilo kuondoka Nchini kwetu ni wajibu wa kila Mwananchi kuhakikisha ananawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni ili kujikinga na magonjwa mbalimbali yanayoletwa na uchafu.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Dkt. Gatete Mahava akinawa mikono kuzindua zoezi la unawaji mikono katika Siku ya Unawaji Mikono Duniani, hafla iliyofanyika katika eneo la Soko la Majengo Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.