JAMII nchini imetakiwa kuondokana na mila potofu zinazomkandamiza mwanamke na kufanya kuonekana mnyonge, asiye na haki na dhaifu ili kuweza kumpa uwezo wa kuonyesha uwezo alionao kwani wanawake ni taifa kubwa.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Chama cha Wanawake Tanzania katika Biashara (TWCC) Taifa, Amina Mpore wakati akisoma risala katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani machi 8 mwaka huu kwa mgeni rasmi Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Dodoma Felista Bura, ambapo aliainisha changamoto ambazo wanawake wamekuwa wakikumbana nazo.
Mpore alisema juhudi za kuwakomboa wanawake zinadidimizwa na jamii kwa kuwa bado wanaendelea kukumbatia mfumo dume katika nyanja muhimu na kumuachia mwanamke mzigo wa malezi ya familia bila kuwa na msaada wa aina yeyote kutokana na mila ambazo hazimruhusu mwanamke kutoa mchango wake.
“Bado wanawake wana kikwazo kikubwa kinachozuia maendeleo yao kuonekana katika jamii, mimba na ndoa za utotoni bado ni changamoto, mtoto wa kike anakabiliwa na changamoto hiyo kubwa, anakosa haki yake ya kimsingi, anakosa kuwa na haki ya kuchagua kipi anakihitaji kwa muda huo, badala yake mila zetu zinamlazimu kuzifuata kutokana na jamii kushindwa kukubaliana na mabadiliko ya kweli ya ulimwengu wa sasa.
“Wanawake bado wanakosa haki ya kurithi ardhi na kumiliki mali, unakuta mwanamke ana familia na mali zake lakini mara tu baada ya mume wake kufariki ananyang’anywa kila kitu anarudishwa nyuma kimaendeleo, anaanza upya wakati alishapiga hatua, jambo hili linakatisha tamaa, linamdumaza mwanamke wa kitanzania na linamfanya anakata tamaa ya maisha”, alisema Katibu huyo.
Pia, alisisitiza suala la mabadiliko kwa jamii, ili kuweza kujenga kizazi imara na chenye mtazamo wa kimaendeleo kwa kuhakikisha wanawake wanapewa kipaumbele kwani kupitia wao jamii inaweza kujengwa vyema ikiwa yenye maadili ama la jamii itaharibika.
“Kauli mbiu ya mwaka huu inasema kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa na ya baadaye, kutokana na kaulimbiu hii jamii ipate mabadiliko ya kweli katika kutekeleza usawa wa kila jambo baina ya mwanamke na mwanaume, ili tuweze kuondokana na mfumo unaompa kipaumbele mwanaume kwa kila jambo.
“Kauli mbiu hii isiishie leo, ikaendelezwe katika jamii yetu tena kwa matendo, mtoto wa kike akaendelezwe kielimu, afanikishe ndoto zake, apewe stadi za maisha ili aweze kujikwamua, apewe na elimu kuhusiana na afya ya uzazi ili aweze kujitambua, tukiyazingatia haya tutatengeneza kizazi bora kijacho, tutawaachia urithi bora watoto wetu tena wa elimu endelevu usiyoharibika”, alisema Mpore.
Risala hiyo ilihitimishwa kwa kuishauri jamii kuondokana na mila potofu, zinazomkandamiza mwanamke hususani ukeketaji pia, imeshauriwa mwanamke apatiwe fursa ya kupatiwa nafasi ya kuonyesha uwezo alionao ili jamii iweze kutambua na kuenzi nafasi yake, jamii, vyama vya siasa, Serikali na asasi za kiraia kutafakari kwa undani mafanikio na changamoto zinazowakabili wanawake katika kuleta maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.