JAMII imetakiwa kutowanyanyapaa wenye ugonjwa Fistula kwani tatizo hilo la kiafya linatibika na huduma ni bila malipo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na watu wenye Ulemavu, Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na wananchi katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Fistula, Mei 23 ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Arusha.
Waziri Dkt. Gwajima amesema, kutokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), nchini Tanzania takribani wanawake 1500-3000 hupata fistula kutokana na matatizo ya uzazi na wanaojitokeza kupata matibabu ni nusu yao tu kwani wengine hujificha kwa kuona aibu na jamii kuwanyanyapaa au kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu huduma.
Waziri Dkt. Gwajima amesema Fistula ni mojawapo ya magonjwa yanayomuondolea mwanamke staha na kumpotezea fursa za kushiriki shughuli za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiroho. Kwa ujumla fistula humtenga mwanamke na maisha ya mwanadamu wa kawaida.
"Matibabu ya fistula ya uzazi nchini mwetu yanatolewa pasipo malipo.
Niwaombe akina baba kuungana katika vita hii ya kutokomeza fistula kwa kuwahamasisha akina mama wenye fistula mnaoishi nao kufika kwenye hospitali ambazo zinatoa matibabu haya bure" amesema Waziri. Gwajima.
Amewahimiza akinamama wajawazito pamoja na wenzi wao kuanza kliniki mapema ili wataalamu wapate muda wa kutambua changamoto na kuchukua hatua kwa wakati.
Amebainisha kuwa, ikiwa imesalia miaka sita ili kufikia azimio la pamoja la nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa la kutokomeza Fistula ifikapo 2030, Tanzania inaendelea kuongeza jitihada na kusisitiza umuhimu wa wajawazito kuanza kuhudhuria kliniki mapema hasa mimba ikiwa na umri chini ya wiki 12, lakini pia kuhakikisha mjamzito anahudhuria angalau mara nne mpaka anafikia kipindi cha kujifungua.
Aidha, amesema miongoni mwa athari kuu za ugonjwa wa Fistula ni kupoteza uwezo wa kudhibiti haja ndogo na kubwa au vyote kwa pamoja bila kuhisi hali inayowafanya baadhi yao kuachwa na waume zao, kunyanyapaliwa pia kutoshiriki shughuli za maendeleo walio wengi hupoteza watoto wao.
Ameongeza kuwa Serikali imewekeza katika Sekta ya Afya kwa kujenga miundombinu pamoja na vifaa vya kutolea huduma za afya.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.