Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepongeza ukarabati wa jengo la utawala na maghorofa mawili ya madarasa katika shule ya sekondari Msalato na kusema kuwa thamani ya fedha inaonekana.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira, Jaffar Mwanyemba alipoongoza Kamati ya Fedha na Utawala (Kundi la Kwanza) kutembelea na kukagua ukarabati wa jengo la utawala na majengo mawili ya ghorofa yenye vyumba tisa vya madarasa shule ya sekondari Msalato mwishoni mwa wiki.
Mwanyemba aliipongeza Kamati ya Ujenzi ya shule na uongozi wa shule kwa kazi nzuri na kusema matumizi ya fedha ni mazuri. Aidha, mkuu wa shule alishauriwa kuomba fedha nyingine kwa ajili ya ukarabati wa majengo mengine ambayo hayafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.
Akisoma taarifa fupi ya ukarabati wa jengo la utawala na majengo mengine mawili ya ghorofa yenye vyumba tisa vya madarasa kwa Kamati ya Fedha na Utawala, Mkuu wa shule ya sekondari Msalato, Mwalimu Neema Maro alisema kuwa shule yake ilipokea shilingi 120,992,215 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la utawala na majengo mawili ya ghorofa yenye vyumba tisa vya madarasa kutoka kwa udhamini wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Mkataba wa ukarabati ulisainiwa kati ya TEA na Mkurugenzi wa Jiji, aliongeza.
Alisema kuwa gharama yote ya mradi ni shilingi 120,992,215, kati ya fedha hizo zimetumika shilingi 120,832,366.14 na kubaki shilingi 159,848.86 kwenye akaunti.
Kuhusu maendeleo ya mradi, Mwalimu Maro alisema kuwa majengo yalitengewa muda wa miezi miwili kwa kila jengo kukamilika. “Hivyo, jengo la utawala lilianza kukarabatiwa mwezi Aprili na kukamilika mwezi Juni. Vyumba tisa vya madarasa ukarabati ulianza mwezi Juni, 2022. Ukarabati wa jengo la utawala pamoja na vyumba vinne vya madarasa (Cookery Block) umekamilika kwa asilimia 100 na majengo yameanza kutumika. Jengo la mwisho (Block 2) nalo lipo katika hatua ya mwisho ya kukamilika kwa sababu mafundi hivi sasa wanamalizia vitu vidogo. Changamoto iliyojitokeza ni ukarabati wa majengo yote haukuweza kuanza kwa pamoja kwa sababu ya uhaba wa vyumba vya madarasa na hivyo, kupelekea kila jengo kukarabatiwa kwa muda wake” alisema Mwalimu Maro.
Jengo la utawala lililokarabatiwa shuleni Msalato.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.