MBUNGE wa Dodoma Mjini, Mhe. Antony Mavunde amesema ujenzi wa hoteli ya nyota nne katikati ya Jiji la Dodoma utachochea maendeleo, biashara na utoaji huduma za kijamii jijini hapo.
Amesema hayo kabla ya Mkurugenzi wa Jiji, Godwin Kunambi na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma kusaini mikataba miwili ya kujenga hoteli ya nyota nne yenye ghorofa 11 na kitega uchumi kwenye mji wa serikali eneo la Mtumba.
Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira alisema ujenzi wa miundombinu ya hoteli na miradi mingine itaongeza chachu ya kuibadilisha Dodoma ambayo miaka iliyopita haikuwa hivi.
Alifafanua kuwa miaka 20 iliyopita Dodoma, mwisho kutembea magari na watu mjini ilikuwa saa mbili usiku, lakini sasa jiji limebadilika unaweza kukutana na watu na magari baada ya muda huo.
Alimpongeza Kunambi kwa ubunifu na ujenzi wa miundombinu, ikiwemo ya hoteli ya nyota nne katikati ya jiji hali inayochochea maendeleo ya jiji ambalo ni makao makuu ya serikali.
Mavunde alisema kuwepo kwa miundombinu ya hoteli kutachochea kukua kwa maendeleo na kuongeza biashara na wakulima wadogo kupata nafasi ya kuuza bidhaa zao na mazao hotelini.
Alibainisha kuwa mkakati wa kujenga hoteli kutaimarisha na kuongeza utalii wa mashamba ya zabibu unaohimizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt Binilith Mahenge.
Amesema ujenzi wa hoteli utaongeza kasi ya utalii na matumizi ya kumbi za mikutano ambazo badala ya watu na taasisi mbalimbali kufanya mikutano jijini Arusha watakuja kufanya jijini Dodoma.
Mavunde alisema ujenzi wa hoteli utachangia maendeleo na siku si nyingi mikutano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) itakuwa ikifanyika Dodoma badala ya Arusha.
Mhe. Mavunde aliipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli akisema maendeleo ya Dodoma yanatokana na juhudi na mkakati wa kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma ambako kumechangia kuongeza mahitaji mbalimbali yakiwemo ya huduma za kijamii.
Alisisitia kuwa kwa kitendho cha serikali kuhamia Dodoma, Baraza la Madiwani wa Jiji limechangamkia fursa hiyo kwa kuazimia kuwekeza katika kujenga hoteli na kitega uchumi katika mji wa serikali.
Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe alisema utiaji saini wa mikataba hiyo miwili unatokana na kujitoa kwa watendaji wa jiji la Dodoma katika kutumia fedha za ndani kwa ufanisi.
Alikazia kuwa, pamoja na huduma hizo za jiji, pia wanatakiwa kupata mikopo kutoka benki mbalimbali mkoani na nchini kutekeleza mikakati hiyo ya kujenga mji wa serikali.
Alisema kwa mikopo hiyo, halmashauri ya jiji la Dodoma itafanikisha azma ya kujenga pia makao makuu ya serikali na kuifanya Dodoma kuwa jiji bora zaidi kwa ubora wa miundombinu.
Chanzo:
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.