HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeshatoa zaidi ya shilingi Bilioni tano kutoka asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kukopesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika jitihada za kuwawezesha kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akifungua mafunzo kwa wajasiriamali watakaokopeshwa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri katika ukumbi wa Shule ya sekondari Umonga.
Mafuru alisema “Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeshatoa shilingi Bilioni tano. Bilioni tano hizi mchango wake ni mkubwa kuliko inavyoweza kutegemewa. Katika msimu huu, tunaingiza kiasi cha Shilingi Milioni 545, ambazo zikiingia katika soko, ndani ya kipindi cha miezi mitatu hadi minne inaweza kuwa imeongeza sana maendeleo, hata kama hairudi kwa Jiji moja kwa moja ila mchango wake unasambaa sana kwa jamii na kuchochea ukuaji uchumi".
Mkurugenzi huyo, aliwataka wanavikundi kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha. “Nisisitize, kwenye vikundi hivi, tunamalezi tofauti na tabia tofauti. Ninachotaka kwenu ni nidhamu ya matumizi na utunzaji wa fedha. Mkifanikiwa ninyi Halmashauri yetu inakuwa imefanikiwa na malengo ya Serikali kufikiwa. Naamini hizi Bajaji na Pikipiki mtaendesha wenyewe, tunachotaka baada ya miezi sita, kama kikundi muweze kuajiri watu wengine ili wengi waweze kunufaika na hiyo shilingi Milioni 545.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeandaa mafunzo kwa vikundi 14 vya wajasiliamali wenye ulemavu, bodaboda na bajaji kabla ya kuvikopesha shilingi Milioni 545.
Awali mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya alipokuwa akimkaribisha Mkurugenzi wa Jiji kufungua mafunzo hayo alisema kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa vikundi vya wajasiriamali ili kuwajengea uwezo wa kuendesha na kusimamia miradi.
“Ndugu Mkurugenzi mafunzo ambayo yanatolewa hapa yanawahusisha wakuu wa idara na wadau toka nje ya Halmashauri. Mweka Hazina wa Jiji ataeleza juu ya usimamizi fedha na uendeshaji wa miradi. Mkaguzi wa Ndani ataeleza juu ya wajibu wa vikundi tunavyovikopesha mikopo kutosababisha kuzalishwa kwa hoja za ukaguzi, ili tusipate hoja mpya” alisema Nabalang’anya.
Eneo lingine ni elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa kumbukumbu ambalo wataalam wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wamejipanga vizuri kufundisha. “Mwanasheria atawaambia kuwa mikopo hii ipo kisheria. Kwa hiyo hata usimamizi wake upo kisheria na siyo mikopo ya kisiasa” alisisitiza Nabalang’anya.
Aidha, alisema kuwa lengo la Mheshimiwa Rais ni kutatua changamoto ya mitaji kwa makundi maalum. Wakati huohuo, kuhakikisha wananchi wa chini wanaimarika kiuchumi. Ndiyo maana baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani ikaondoa riba. Mikopo hii ilikuwa inahudumia makundi mawili tu, wanawake na vijana ila baada ya Serikali hii kuingia madarakani ikaongeza kundi la watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake mnufaika wa mikopo hiyo, Lucy Ndahani aliishukuru Serikali kwa kutoa mikopo hiyo. “Napenda kutoa heshima kwa Mkurugenzi wa Jiji kututembelea, tunamshukuru sana kutujali sisi wanawake wenye ulemavu na kuwajali vijana na wanawake. Tunatoa shukrani kwa Rais Magufuli kututengea fedha kwa ajili ya kujiendeleza. Namshukuru sana Mungu kutupa viongozi hawa wema, namuomba Mungu awabariki sana” alisema Ndahani kwa hisia kali.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya alipokuwa akiongea kumkaribisha Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kufungua mafunzo.
Wanufaika wa mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10 wakimsikiliza Mkurugenzi wa Jiji (hayupo pichani) alipokuwa akifungua mafunzo kwa wajasiriamali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.