HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imesaini mikataba ya ujenzi wa miradi ya kimkakati yenye thamani ya shilingi bilioni 69.29 katika jitihada zake za kuelekea kujitegemea kimapato.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akitoa maelezo mafupi ya miradi ya kimkakati ya ujenzi wa hoteli ya Jiji la Dodoma na jengo la kitegauchumi la Jiji katika halfa ya utiaji saini mikataba miwili ya miradi ya uwekezaji Nyerere square leo.
Kunambi alisema kuwa Halmashauri ya Jiji inasaini mkataba wa ujenzi wa Hoteli ya Jiji la Dodoma (Dodoma City Hotel) itakayojengwa katika mtaa wa Nyerere na Mkandarasi Stecol Coorporation (China) kwa gharama ya shilingi bilioni 9.995. Alisema kuwa hoteli hiyo itakayokuwa na hadhi kati ya nyota tatu na nyota nne, itakuwa na ghorofa 11 ikiwa na kumbi za mikutano, mgahawa mkubwa, vyumba vya kulala na maegesho ya magari.
Mkataba wa pili aliutaja kuwa ni ujenzi wa jengo la kitegauchumi la Jiji (Government City Complex) litakalojengwa katika Mji wa Serikali – Mtumba. Jengo hilo litajengwa na Mkandarasi Mohamed Builders Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 59.3. “Jukumu la Halmashauri ya Jiji ni kujenga makao makuu ya nchi. Hivyo, awamu ya kwanza litajengwa jengo la ghorofa sita litakalokuwa na mgahawa, sehemu za taasisi za kifedha, na kumbi za mikutano zenye ukubwa tofauti na ‘apartments kwa gharama ya shilingi bilioni 18’” alisema Kunambi.
Miradi yote itajengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri. “Halmashauri ya Jiji tunataka ku-cross border kwenda mikoa mingine kuwekeza na hadi nje ya nchi. Fedha zipo ni fikra sahihi na uzalendo tu. Ndani ya mwaka mmoja watakabidhi miradi yetu” alisema Kunambi.
Katika salamu za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo aliipongeza Halmashauri ya Jiji kwa ukusanyaji mapato ya ndani. “Hakuna Halmashauri yeyote nchini iliyoweza kukusanya shilingi bilioni 71. Halmashauri nyingine zinakusanya shilingi bilioni mbili na nyingine shilingi bilioni 30 kwa mwaka. Ninyi mnaweza kuwalipa mishahara na kuwatekelezea miradi ya maendeleo Halmashauri zingine mbili” alisema Jafo.
Nae mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dkt Binilith Mahenge alisema kuwa Dodoma, inakabiliwa na changamoto ya uwekezaji katika shule za kimataifa, na kualika wawekezaji katika eneo hilo. Akiongelea ujenzi wa miradi ya kimkakati ya Halmashauri ya jiji, aliitaja kuwa ni sawa na ujenzi wa viwanda. “Hoteli hiyo ni sawa na kiwanda, utapata matumizi ya bidhaa zinazotoka Dodoma. Ukitumia mvinyo unamhamasisha mkulima wa zabibu kulima zaidi” alisema Dkt Mahenge.
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo akitoa nasaha kwa wakandarasi baada ya tukio la kusaini mikataba ya Ujenzi wa Majengo ya Vitegauchumi vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini leo.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe (wa pili kulia waliokaa) na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (wa kwanza kulia waliokaa) wakiweka saini kwenye mtakaba wa Ujenzi wa 'Government City Complex' pamoja na wawakilishi wa Kampuni ya Mohamed Builders Ltd.
Mgeni rasmi wa tukio la utiaji saini wa Mikataba ya Ujenzi wa Majengo ya Vitegauchumi vya Jiji la Dodoma Mhe. Selemani Jafo (wa nne kutoka kushota waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (wa tatu kushoto waliokaa), Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma (wa tatu kulia waliokaa), Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (wa kwanza kulia waliokaa), Mbunge wa Jimbo la Dodoma (wa pili kulia waliokaa), wawakilishi wa Wakandarasi wa miradi ya vitegauchumi na viongozi mbalimbali waliohudhuria halfa ya utiaji saini miradi ya Jiji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.