HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeanza utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli la kuwalipa wananchi zaidi ya 1,500 ambao ardhi yao ilitwaliwa kupisha ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi ya Taifa katika Kata ya Kikombo jijini hapa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa agizo la Rais la kuwalipa fidia wananchi wa Kikombo katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji leo.
Kunambi amesema “tarehe 25 Novemba, 2019, Mhe Rais alitoa agizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauriya Jiji la Dodoma kulipa fidia kwa wananchi 1,526 walioachia maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi ya Taifa. Kiasi cha fidia kitakacholipwa ni shilingi biliobi 3.399. Fedha hizi zipo, tumeshaziratibu na tayari kulipwa kama Mhe. Rais alivyoelekeza”. Zoezi la uhakiki limekamilika na anatarajia kuwasilishiwa taarifa hiyo wiki hii.
Kufuatia agizo la Rais, Halmashauri ya Jiji la Dodoma tarehe 26 Novemba, 2019 ilianza utekelzaji wa agizo hilo kwa kuwaelekeza watendaji kuwasaidia wananchi ambao hawakuwa na akaunti za benki kuweza kufungua akaunti kwa ajili ya malipo.
Aidha, amemshukuru Rais, kwa kazi nzuri anayoifanya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu na barabara. “Napenda kumshukuru sana Mhe Rais kwa kuagiza ujenzi wa barabara ya km 18 kwa kiwango cha lami kuelekea Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa. Kikombo ndiyo mji mpya wa Dodoma” alisema Kunambi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.