HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeibuka na jawabu la kuwafanya wanafunzi kutozurura kipindi cha mapumziko ya mapambano ya virusi vya Corona na kuwanufaisha kielimu.
Jawabu hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma juu ya mkakati wa Jiji hilo kuwafundisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kipindi cha mapumziko ya mapambano ya Covid-19.
Mkurugenzi Kunambi amesema kuwa kufuatia agizo la serikali kufunga shule za msingi na sekondari nchini, wanafunzi wapo nyumbani. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma tunasema maisha lazima yaendelee na wanafunzi wasome wakiwa nyumbani. Kipindi hiki wanafunzi wengi wapo nyumbani ila changamoto kubwa ni uzururaji mtaani kwa sababu hawana kazi za kufanya nyumbani. Tumekuja na jawabu la kuwafanya wasizurure kwa kuwaanzishia vipindi katika redio zilizopo ndani ya Jiji la Dodoma” amesema Kunambi.
Mkurugenzi huyo amezipongeza redio za Dodoma kwa mwitikio chanya wa kutoa vipindi kwa ajili ya kuwafundishia wanafunzi. “Ndugu zangu hizi ni redio za mfano na za kizalendo kweli. Ushirikiano huu ni muhimu kwa manufaa ya wanafunzi wa Jiji letu la Dodoma, na niwahakikishie hatutawaangusha” alisisitiza Kunambi.
Kwa upande wake Afisa Elimu ya Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Upendo Rweyemamu amesema kuwa katika vipindi vitakavyofundishwa ni masomo yote ya Kidato cha Pili na cha Nne. Walimu wabobezi 26 wameandaliwa na ratiba ya vipindi hivyo itawekwa katika tovuti ya Halmashauri, aliongeza.
Nae Afisa Elimu ya Msingi wa Jiji la Dodoma, Mwl. Joseph Mabeyo amesema kuwa katika darasa la nne masomo sita yatafundishwa. “Kwa wanafunzi wa darasa la saba, masomo yatakayofundishwa ni matano. “Walimu wameandaliwa vizuri na mada zipo tayari kwa ajili ya wanafunzi” amesema Mwl. Mabeyo kwa kujiamini.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina jumla ya shule za msingi 133 zenye jumla ya wanafunzi 113,441 na shule za Sekondari 56 zikiwa na wanafunzi 30,785.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (katikati) akiongea na vyombo vya habari kuhusu mkakati wa Jiji la Dodoma kusaidia wanafunzi walio nyumbani kufuatia agizo la Serikali kuzifunga shule zote za msingi na sekondari kutokana na janga maambukizi ya virusi vya Corona nchini. Kushoto ni Afisa Elimu ya Sekondari wa Jiji la Dodoma Mwalimu Upendo Rweyemamu na kulia ni Afisa Elimu ya Msingi wa Jiji la Dodoma Mwalimu Joseph Mabeyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.