TIMU ya kimkakati ya masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekaribishwa wilayani Mufindi kuvutia wawekezaji kwenda kuwekeza jijini Dodoma na kukuza uchumi wa taifa.
Ukaribisho huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri Willian alipokutana na kufanya mazungumzo na timu ya kimkakati ya masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipofika kumsalimia ofisini kwake mjini Mafinga.
William alisema “mimi niwakaribishe sana Mufindi kuangalia fursa za uwekezaji kwenye wilaya yetu kwa sababu wawekezaji wakiwekeza Jiji la Dodoma wanakuwa wamewekeza Tanzania, wakiwekeza Mufindi wanakuwa wamewekeza Tanzania. Najua uwekezaji unategemea sana vivutio vilivyopo eneo husika”.
Akiongelea dhana ya uwekezaji, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa uwekezaji ni ushirikiano wa pande zaidi ya moja. “Katika uwekezaji tunategemeana, sisi tunajitahidi kuvutia wawekezaji Mkoa wa Iringa, lakini uwekezaji unakuwa kwenye mnyororo wa thamani. Sisi zao letu kubwa Mufindi ni mbao na bidhaa zinazotokana na misitu. Tunatengeneza bidhaa za misitu na ndiyo maana tuna viwanda vingi vya mazao ya misitu. Tunakiwanda kikubwa cha karatasi na malighafi mkubwa ni mbao” alisema William.
Aidha, alisema kuwa zikipigwa hesabu za kiuchumi, tayari kuna wawekezaji wa Mufindi ambao wamewekeza Jijini Dodoma. Alikitolea mfano kiwanda cha Sao Hill ambacho kina tawi jijini Dodoma wakipasua na kutibu mbao.
Akiongelea fursa ya hali ya hewa ya Mufindi kwa kilimo cha mbogamboga na uwekezaji katika Jiji la Dodoma, Mkuu huyo wa Wilaya alisema “sisi kwa hali ya hewa tuliyonayo, tunaweza kuzalisha matunda na mbogamboga na kuziuza jijini Dodoma mwaka mzima. Hivyo, hii ni fursa ya kuwekeza katika eneo hilo. Nafahamu kuwa Serikali inajenga uwanjwa mkubwa wa kimataifa wa Ndege wa Msalato utakaowezesha hata kusafirisha nje ya nchi mbogamboga na matunda kutoka Mufindi”.
Akimuelezea fursa za uwekezaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Afisa Maendeleo ya Jamii katika Jiji hilo, Zainab Manyike alisema kuwa Jiji hilo limepima na kutenga viwanja vya matumizi mbalimbali katika maeneo tofauti.
“Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepima viwanja vya viwanda katika Kata ya Nala, eneo hilo vinaweza kujengwa viwanda vya kuchakata mazao ya misitu. Hii ni fursa kwa wananchi wa wilaya Mufindi kuwekeza jijini Dodoma. Aliongeza kuwa wawekezaji wa wilaya ya Mufindi wanaweza kujipanga kunufaika na ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa Msalato Jijini Dodoma ili kuweza kusafirisha mazao ya matunda na mbogamboga ndani na nje ya nchi” alisema Manyike.
Awali akielezea lengo la ziara hiyo wilayani Mufindi, Afisa Habari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe, alimtaarifu Mkuu huyo wa Wilaya kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeamua kutoka ofisini na kuwafuata wawekezaji katika maeneo yao. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma tunafahamu kuwa wawekezaji ni watu wenye majukumu mengi na muda mchache, hivyo tumeamua kuwaondolea usumbufu wa kwenda kutafuta maeneo ya kuwekeza Jiji la Dodoma kwa kuwaletea fursa hizo wilayani Mufindi” alisema Gondwe.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William (kulia) akiwaonesha wajumbe wa timu ya masoko ya kimkakati ya Jiji la Dodoma jinsi mabaki ya mbao yanavyounganishwa na kutengeneza samani wilayani Mufindi
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.