Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepima viwanja zaidi ya 800,000 katika kipindi cha miezi 30 ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha jiji linapimwa na wananchi kuishi katika maeneo yaliyopimwa na kupangwa kitaalam.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akifafanua hoja katika kikao baina ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini hapa.
Mkurugenzi Mafuru alisema “Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) iliyofanya kazi kwa miaka 43 ilifanikiwa kupima na kumilikisha viwanja 69,000. Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kipindi cha miaka miwili na nusu imefanikiwa kuzalisha viwanja zaidi ya 800,000. Haya ni mafanikio makubwa katika sekta ya ardhi. Baada ya viwanja vingi kuwa vimepimwa na kumilikishwa kwa wananchi, changamoto kubwa iliyopo ni jinsi ya kufika katika viwanja hivyo. Katika kutatua changamoto hiyo, tumeagiza mitambo mipya kwa ajili ya kufungua barabara. Tuna mitambo yetu minne japo inachechemea lakini inaendelea kufanya zoezi la kufungua barabara”.
Aidha, alisema kuwa halmashauri yake imeagiza vifaa vya upimaji seti nne mpya kwa ajili ya kazi ya upimaji ardhi. “Lengo la kuagiza vifaa hivyo ni kuwatumia wataalam wetu wa upimaji ili wafanye kazi kwa ufanisi, muda mfupi na kwa gharama nafuu. Utumishi wa umma ni kutumikia watu, siwezi sema ‘I am very busy’ hapana” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amepanga kufanya vikao na halmashauri zote nane za Mkoa wa Dodoma kuongea na watumishi ili kuweka dira ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya mkoa huo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.