HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli za washirikisha wananchi katika kujenga uchumi kwa kutoa mikopo ya thamani ya shilingi 545,000,000 kutoka mapato yake ya ndani katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020/2021.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge katika halfa fupi ya kukabidhi mikopo ya asilimia 10 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vikundi iliyofanyika katika uwanja wa Nyerere ‘Square’ jijini hapa.
Dkt. Mahenge alisema “leo tunashuhudia Rais, Dkt. John Magufuli akiwashirikisha wananchi na makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika shughuli za kiuchumi. Baada ya utaratibu huu wa mikopo ya asilimia 10 utekelezaji wake kusuasua, serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani ikatunga sheria. Sheria hii imerahisisha utekelezaji wake. Leo kijana anayekabidhiwa bodaboda anakuwa ametatuliwa changamoto ya usafiri, nae kushiriki katika kutatua changamoto za watu wengine kwa kuwasafirisha. Hivyo kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi”.
Alisema kuwa serikali na makao makuu ya nchi kuhamishiwa Dodoma, kumelifanya Jiji la Dodoma kukua kiuchumi. “Ndugu zangu, matunda na makao makuu ya nchi kuhamia Dodoma, Jiji la Dodoma ndiyo Halmashauri pekee inayotenga na kukopesha fedha nyingi kwa wakundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Haya ni matokea ya serikali kuhamia Dodoma na utendaji kazi nzuri wa Jiji la Dodoma” alisema Dkt. Mahenge.
Alisema kuwa leo atakabidhi bajaji na bodaboda kwa makundi hayo, na kuwataka kuvitunza. “Ombi langu kwenu mnaopokea vifaa hivi au hundi, hii ni fursa kubwa kwenu hakikisheni mnavitunza ili viwaletee maendeleo yaliyokusudiwa” alisema Dkt. Mahenge.
Akiwasilisha taarifa ya utoaji mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa Halmashauri yake imetoa zaidi ya shilingi bilioni tano kuvikopesha vikundi. “Kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020, mikopo iliyotolewa kwa makundi hayo ni shilingi 5,292,829,899. Vikundi 812 vya wanawake vimenufaika na shilingi 3,254,962,583, vikundi 425 vya vijana vimenufaika na shilingi 1,856,537,316 na vikundi 30 vya watu wenye ulemavu vimenufaika na shilingi 181,330,000” alisema Mafuru.
Jumla ya vikundi vyote vilivyopata mikopo ni 1,267 vikiwa na wanavikundi 12,670, aliongeza.
Akiongelea ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo hiyo, alisema kuwa unaendelea vizuri. “Hadi kufikia mwezi Septemba, 2020 kati ya shilingi 5,292,829,899 zilizokopeshwa, shilingi 2,526,769,984 zimerejeshwa na kiasi kilichobaki ufuatiliaji unaendelea” alisema Mafuru.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetenga jumla ya shilingi 2,262,708,770 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. “Katika robo ya kwanza Julai-Septemba, 2020, Halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 545,000,000. Vikundi saba vya wanawake shilingi 125,000,000, vikundi viwili vya vijana shilingi 378,000,000 na watu wenye ulemavu shilingi 42,000,000. Vikundi hivyo, vimekopeshwa ili kutekeleza miradi ya usafirishaji kwa njia ya bodaboda na bajaji, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ujenzi wa machinjio ya kuku, utengenezaji wa bidhaa za Ngozi, saluni na ushonaji” alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang’anya alimshukuru Rais kwa kuifanya mikopo hiyo kuwa kisheria. “Kabla ya serikali ya awamu ya tano, mikopo hii haikuwa kisheria hivyo utekelezaji wake ulikuwa unasuasua, baada ya serikali hii kuingia madarakani ilitunga sheria na kuifanya mikopo kuwa kisheria. Awali mikopo hii ilikuwa kwa ajili ya makundi mawili, wanawake na vijana, lakini serikali hii ilipoingia madarakani imeongeza kundi la watu wenye ulemavu. Wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili” alisema Nabalang’anya.
Nae mnufaika wa mikopo hiyo, Mariam Ally kutoka kikundi cha Muwakiki kilichopo Kata ya Tambukareli jijini hapa alishukuru kwa niaba ya vikundi vyote. “Shukrani kwa niaba ya vikundi vyote kwa Jiji la Dodoma, tunashukuru sana kwa uwepo wa mikopo isiyokuwa na riba. Tunamshukuru sana Rais, Dkt. John Magufuli na tunaomba aendelee kuwanufaisha wengine, tunaushukuru uongozi wa Jiji la Dodoma kutusimamia tumepata mikopo na baadhi tumerudisha mikopo hiyo” alisema Ally.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Sharifa Nabalang'anya akitoa maelezo ya awali wakati wa hafla ya kuwakabidhi wajasiliamali mikopo ya asilimia 10 ambapo pia alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kuifanya utoaji wa mikopo ya hiyo kuwa sheria.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (mwenye suti katikati) akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi Milioni 545 kwa vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu kwenye hafla iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyerere Square Jijini Dodoma, kulia kwa Mkuu wa Mkoa ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru na kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Makuka Kessy, kushoto kabisa ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Jiji la Dodoma Sharifa Nabalang'anya na wengine ni miongozi mwa wanufaika wa mikopo hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.