Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejipanga kutoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo (machinga) na mama lishe katika kituo kikuu cha mabasi cha kimataifa cha Dodoma mkoani humo.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya kukamilika kwa mchakato wa kuwapata wafanyabiashara katika maeneo ya kituo kikuu cha mabasi Dodoma na soko kuu la Job Ndugai leo.
Kunambi amesema kuwa Halmashauri ya Jiji imeweka utaratibu mzuri wa kuratibu machinga na mama lishe katika kituo hicho ili waweze kufanya biashara bila usumbufu wowote. Hii ni kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kutenga eneo maalumu kwa makundi hayo muhimu kufanya biashara, ameongeza.
“Machinga ni sehemu ya hii stendi hivyo, tumetenga maeneo mawili tofauti kwa ajili ya machinga ambayo kila eneo linauwezo wa kukaa machinga 300. Eneo la mama lishe lina uwezo wa kuchukua watu 30, na tumetoa kipaumbele kwa akina mama walio katika stendi ya sasa ya mabasi ya Nanenane. Hatuwezi kuwaacha, lazima tuhame nao. Wakija hapa ni lazima wabadilike kwasababu ni eneo la kisasa” amesema Kunambi.
Hata hivyo ametoa rai kwa wafanyabishara hao kuwa makini na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa sheria ikiwa ni pamoja na kutoingia katika maeneo ambayo hawaruhusiwi. Aidha, alisisitiza kuwa wataratibiwa vizuri ili wazingatie usafi na utunzaji wa maeneo ya kufanyia biashara katika stendi hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.