HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepima zaidi ya viwanja 200,000 katika kipindi cha miaka miwili na miezi nane tofauti na viwanja 69,000 vilivyopimwa na iliyokuwa Mamlaka ya Ushawishaji Makao Makuu (CDA) kwa kipindi cha miaka 43.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akitoa maelezo ya utendaji kazi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa jiji hilo leo.
Kunambi amesema “katika sekta ya ardhi tupo mbali, katika kipindi cha miaka miwili na miezi nane Halmashauri ya Jiji imepima viwanja zaidi ya 200,000. Viwanja 135,000 wananchi wamekabidhiwa barua za kupata viwanja hivyo. Haya ni mafanikio makubwa ikilinganishwa na CDA iliyopima viwanja 69,000 katika kipindi cha miaka 43”. Alisema kuwa kati ya viwanja vilivyopimwa na CDA, viwanja 12,000 zilitolewa barua za kupewa viwanja hivyo wakati hati zilizotolewa ni 25,000. “Viwanja zaidi ya 8,000 vilikabidhiwa kwa wananchi bila kukamilika hatua za upimaji wake” ameongeza Kunambi.
Akiongelea upimaji katika Halmashauri ya Jiji hilo, Kunambi amesema kuwa kila eneo katika Jiji la Dodoma limepimwa. “Mgeni yeyote anayenunua ardhi bila kufuata utaratibu, afahamu kuwa anaibiwa kwa sababu ananunua eneo lililopangwa tayari. Lazina anayetaka kununua ardhi eneo la Jiji la Dodoma afanye mawasiliano na Halmashauri ambayo ndiyo mamlaka ya upangaji mji” amesema Mkurugenzi Kunambi.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma amefanya ziara ya kawaida katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujitambulisha pamoja na kuongea na timu ya Menejimenti ya Halmashauri.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi akitoa taarifa fupi kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Jiji la Dodoma mbele ya mkuu mpya wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Josephat Maganga na timu yake pamoja na timu ya manejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma (CMT) leo 11 Agosti 2020 katika ukumbi mdogo Makao makuu ya Ofisi za Jiji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.