HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeamua kutoka ofisini na kuwafuata wagonjwa wa kifua kikuu na kuwaanzishia tiba katika mkakati wa kupambana na maambukizi mapya kwa jamii.
Mkakati huo ulitajwa na mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Peres Lukango (pichani) alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake leo jijini Dodoma.
Dkt. Lukango alisema kuwa Halmashauri ya Jiji imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ugonjwa wa kifua kikuu. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kukabiliana na ugonjwa wa kifua kikuu, tumeamua kutoka ofisini na kuwafuata washukiwa wa ugonjwa wa kifua kikuu huko walipo. Tofauti ya zamani tulikuwa tunawasubiri wagonjwa waje katika vituo vya afya. Sasa hivi, tunawatafuta, kuwafikia, kuwachunguza na wanapobainika tunawaanzishia huduma ya matibabu hadi wapone” alisema Dkt. Lukango. Njia hiyo inasaidia kuwafikia wagonjwa wengi kwa sababu wengine hukosa nauli ya kwenda katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi, aliongeza.
Halmashauri imekuwa ikitumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwenye mapambano dhidi ya kifua kikuu. Wahudumu hao wamekuwa wakiwasaidia wagonjwa wa kifua kikuu katika huduma za tiba.
Mratibu huyo alisema kuwa elimu imeendelea kutolewa katika Halmashauri ya Jiji ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na elimu ya kujikinga na ugonjwa wa kifua kikuu. “Madaktari wa pembezoni tumewajengea uwezo wa kubaini wagonjwa wa kifua kikuu wanapofika katika vituo vyao. Njia bora ya kubaki salama ni kutibu ugonjwa huo” alisema mratibu huyo. Vilevile, aliitaka jamii kuhakikisha nyumba na maeneo ya kazi yanakuwa na hewa ya kutosha inayozunguka na mwanga kwa sababu mwanga unasaidia kuua vimelea vya kifua kikuu.
Elimu inayoendelea kutolewa inajikita katika kuyalinda makundi ambayo yapo katika hatari ya kupata ugonjwa huo. Aliyataja makundi hayo kuwa ni wazee kutokana na kinga zao kuwa zinashuka. Kundi lingine ni watoto wadogo kutokana na kinga zao kuwa hazijakomaa. Makundi mengine ni watu wanaougua magonjwa sugu kama kisukari, saratani na utapiamlo.
Aidha, aliwashukuru wafadhili wanaofadhili upatikanaji wa dawa hizo. “Shukrani kwa wafadhili wa kifua kikuu, kwa sababu wanawezesha dawa hizo kutolewa bure kwa wagonjwa. Unajua matibabu ya kifua kikuu ni miezi sita, hivyo ni gharama kubwa kama mgonjwa angekuwa ananunua dawa hizo mwenyewe. Ugonjwa huu bahati mbaya zaidi unawaathiri zaidi watu wa kipato cha chini na uwezo wa kufanya kazi unapungua sana” alisema Dkt. Lukango.
Akiongelea hali ya kifua kikuu katika Jiji la Dodoma, Dkt. Lukango alisema kuwa mwaka 2019 halmashauri iliwekewa lengo la kuibua wagonjwa zaidi ya 1500 na wagonjwa walioibuliwa ni zaidi ya 1450 lengo hilo lilifikiwa kwa asilimia 90. “Mwaka 2020 tumepewa lengo la kuibua wagonjwa zaidi ya 2000 likiwa ni lengo kubwa kuliko Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma. Hadi sasa tumeibua wagonjwa zaidi ya 430 na juhudi zinaendelea vizuri” alisema Dkt. Lukango.
Nae Dkt. Raymond Ndolele alisema kuwa wagonjwa wanaopatikana na kuanza matibabu hufuatiliwa hadi wamalize matibabu. “Wagonjwa tunaowapata huwa tunafanya ufuatiliaji kwenye familia zao ili kubaini kama wameambukiza watu wengine ili wote waanze matibabu ya kuwakinga.
Kwa upande wake muuguzi Foibe Nonya alisema kuwa wagonjwa wa kifua kikuu wanaohudumiwa dozi ya kwanza ni miezi mwili, na kuendelea na miezi minne inayobaki.
Muhudumu wa afya ngazi ya jamii, Rose Lema alisema kuwa wamekuwa wakitoa elimu ya lishe kwa wagonjwa wa kifua kikuu ili kuwasaidia kuwa na afya njema katika kipindi chote wanachoendelea na matibabu.
Maadhimisho ya siku ya mapambano ya kifua kikuu mwaka 2020 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Wakati ni huu, tuunganishe nguvu na kuwajibika katika mapambano ya kutokomeza kifua kikuu”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.