HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetakata katika mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari (UMISSETA) ngazi ya mkoa kwa kuibuka mshindi wa jumla katika mashindano hayo na kubeba makombe 9 katiya 12 yaliyokukwa yakigombewa katika michezo mbalimbali.
Akiongelea siri ya ushindi huo, Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alisema kuwa ushirikiano ndiyo msingi wa mafanikio hayo.
“Ninayo furaha kubwa sana kwa matokeo ya leo ya UMISSETA. Tumekuwa hapa tukishindana na Halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma na Jiji la Dodoma tumeibuka kidedea kwa kuibuka na makombe 9 kati ya makombe 12 yaliyoshindaniwa. Nawashukuru sana walimu wangu wa michezo ambao wamewaandaa wanafunzi hawa katika ngazi ya shule, kata, tarafa na ngazi ya wilaya na hatimaye sasa katika ngazi ya mkoa. Ninawapongeza sana walimu wa michezo kwa kupambana. Ninawashukuru wakuu wangu wa shule wa Dodoma Jiji pamoja na Maafisa Elimu Kata kwa kunitia moyo na tumekuwa tukishauriana sana. Hivyo, umoja wetu ndiyo umetusababishia ushindi huu mkubwa” alisema Mwalimu Rwenyemamu.
Timu ya UMISSETA ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imebeba vikombe tisa, katika michezo ya mpira wa mikono (wasichana), mpira wa mikono (wavulana), mpira wa wavu (wasichana), mpira wa miguu (wasichana), mpira wa pete, mpira wa kikapu (wasichana), mpira wa kikapu (wavulana), kwaya na ushindi wa jumla ya mashindano yote.
Timu ya UMISSETA Mkoa wa Dodoma itaweka kambi kwa muda wa wiki moja kujiwinda na mashindano ya kitaifa yatakayofanyika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Kwa upande wake, kapteni wa timu ya mpira wa kikapu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyoibuka na kombe la mchezo huo, Gervas Fred alisema kuwa siri ya mafanikio ni ushirikiano na kucheza kwa umoja kama timu. Alisema kuwa mafunzo mazuri ya kocha wao yalikuwa chachu ya mafanikio katika michezo yote waliyoshiriki.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.