MAMLAKA ya Maji safi na usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) imetoa ndoo 40 za kunawia mikono pamoja na mifuko miwili ya sabuni katika kuunga mkono vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona Nchini.
Meneja ufundi wa DUWASA ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo Mhandisi Kashirimu Mayunga amesema kuwa wameamua kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kupambana na gonjwa hilo hatari ambalo ni janga la Dunia kwa sasa.
“Tumetoa ndoo hizi arobaini na mifuko miwili ya Sabuni ambayo wao kama Jiji wataangalia wenyewe wataweka wapi ndoo hizo ili kusaidia wana Dodoma kujikinga na ugonjwa huu hatari” alisema Mayunga.
Wakati akipokea vifaa hivyo, Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu Jiji la Dodoma Dickson Kimaro alisema kuwa, wao kama Jiji watahakikisha vifaa hivyo vinatumika ipasavyo ili kujikinga na maambukizi ya Ugonjwa wa COVID-19 ambao tayari umeingia nchini.
“Tunasema asante sana kwa wenzetu wa DUWASA kwa kutupatia ndoo arobaini na mifuko miwili ya sabuni vifaa ambavyo vitasaidia sana kupambana na ugonjwa huu ndani ya Jiji la Dodoma” alisema Kimaro.
Mkuu huyo wa Idara ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi, alitoa wito kwa wadau wengine Jijini humo kujitokeza kuunga mkono kwa vitendo juhudi za kupambana na janga hilo kwa kusaidia makundi mbalimbali yenye mahitaji ikiwemo kutoa vifaa vya kujikinga na kujisafisha.
Meneja Ufundi wa DUWASA, Kashirimu Mayunga (kulia) akimkabidhi ndoo Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro (kushoto) aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma.
Ndoo arobaini (40) zilizotolewa na DUWASA kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 katika Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.