Na Nemes Michael, DODOMA
SHIRIKA la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Halmashari ya Jiji la Dodoma wameahidi kutatua changamoto za miundombinu ya maji katika mradi wa umwagiliaji, na upatiknaji wa elimu stahiki ya kupambana na wadudu katika kata ya Kikombo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi Msaidizi Mkazi wa shirika hilo nchini Tanzania Charles Tulai wakati wa makabidhiano ya mbegu bora kwa wakulima wa kikundi cha Ilolo kilichopo mtaa wa Kikombo Makulu pamoja na pikipiki kwa Afisa Kilimo wa kata ya Kikombo.
Akizungumza katika mkutano huo, Tulai alisema kuwa ushirikiano walionao na Halmashairi ya Jiji la Dodoma ni mkubwa na wenye lengo la kuhakikisha utekelezaji chanya wa shughuli katika sekta ya kilimo.
“Ulaji katika dunia nzima hasusan ya ulimwengu wra tatu huku Afrika, bado hatujafikia hatua ya lishe inayotakiwa, tunasahau vitu muhimu kama matunda na mboga, hichi kikundi kimenifanya nije kwa sababu kimenipa hamasa na naamini wengi watajifunza kupitia kwenu, hakika mnastahili pongezi” alisema Tulai.
Tulai aliongeza kuwa, mbegu zilizoletwa ni mbegu sahihi katika kuhakikisha tunaboresha afya zetu binafsi na vipato vyetu, na kwa hatua hii naamini wakulima wa Kikombo Makulu watakuwa mfano kwa wakulima wengine katika kilimo kisichotegemea mvua na chenye mavuno ya kutosha.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Jiji la Dodoma, Yustina Munishi ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Jiji hilo Joseph Mafuru, aliliishukuru FAO na kwamba ushirikiano ulipo baina ya taasisi hizo umekuwa mzuri na wenye mafanikio.
“Ushirikiano huu ni wa muda na wenye mafanikio, hatua tulizofikia kwa kuleta mbegu sahihi na elimu katika kilimo cha umwagiliaji ni hatua nzuri katika kuhakikisha tunatetea afya za wananchi na kuongeza kipato binafsi cha mkulima na Taifa kwa ujumla” alisema Munishi.
Naye, Afisa Kilimo Kata ya Kikombo Madei Kidarya alilishukuru shirika la FAO na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kukabidhiwa pikipiki ambayo itamsaidia katika usafiri na urahisishaji wa huduma kwa wakulima wa kata hiyo.
Mmoja wa wanakikundi cha wakulima kilichonufaika na mbegu hizo Martha Ramadhani alisema kuwa, hapo awali hali haikuwa sawa kutokana na aina ya mbegu zilizokuwa zinatumika, ila sasa kupitia mbegu bora walizokabidhiwa anaamini kutakuwa na maendeleo chanya katika kuimarisha afya na kuinua uchumi kwa wakulima na Taifa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.