Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kuwa kinara katika utengaji fedha kwa ajili ya masuala ya lishe katika mkakati wake wa kukabiliana na udumavu.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipoongoza kikao cha Kamati ya Ushauri Wilaya ya Dodoma kujadili mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Shekimweri alisema “nimefurahi kuona mmetenga fedha kwenye bajeti kwa masuala ya mkataba wa lishe shilingi 1,000, na mimi nitumie nafasi hii kuwapongeza Halmashauri ya Jiji. Mkurugenzi wa Jiji na wakuu wa divisheni hamjasema tu, nijuavyo jiji hutenga zaidi ya shilingi 1,000 hutenga kati ya shilingi 1,200 hadi 1,300 hili nawapongeza na lisimamiwe na mkiweza muongeze zaidi”.
Alisema kuwa lishe ina mchango mkubwa katika ufanisi wa elimu ya wanafunzi. “Tumekuwa tukitoa msisitizo wa elimu ila kama hatushughuliki na lishe hatuwezi kufanikiwa. Kwa Dodoma kiwango cha udumavu ni asilimia 33, lazima tukishushe kiwango hiki. Hivyo, afua hizi zitasaidia sana” alisema Shekimweri.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imekadiria kukusanya na kutumia mapato yenye jumla ya shilingi 128,278,555,369 kutoka vyanzo katika vyanzo vyake vya ndani, serikali kuu, wahisani kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo, utoaji huduma na kujiendesha.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.