HALMASHAURI ya jiji la Dodoma imepanga kuwafikia watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano na kuwapatia huduma ya matone ya vitamin ‘A’, dawa za minyoo na upimaji hali ya lishe katika mwezi Juni ambao ni mwezi wa afya na lishe ya mtoto.
Kauli hiyo imetolewa na afisa lishe wa Halmashauri ya jiji la Dodoma, Semeni Juma alipokuwa akielezea jiji lilivyojipanga katika kutekeleza mwezi wa afya na lishe ya watoto ofisini kwake leo.
Juma amesema kuwa katika mwezi wa afya na lishe ya mtoto ambao huwa mwezi wote wa Juni nchini, Halmashauri ya jiji itaendesha kampeni itakayohusisha huduma ya utoaji matone ya vitamin ‘A’, dawa za minyoo na upimaji wa hali ya lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Lengo ni kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wanakuwa na afya njema na kuepukana na matatizo ya lishe yanayotokana na ukosefu au upungufu wa vitamin A, minyoo na utapiamlo, aliongeza.
Juma aliwataka wazazi na walezi wote kuhakikisha watoto wao wenye umri wa chini ya miaka mitano wanapata fursa hiyo. “Nia ya serikali ni kuhakikisha watoto wote wanapata huduma bora za kiafya. Mwezi huu wa wa afya na lishe umelenga kuhakikisha watoto wote wanapata huduma ya matone ya vitamin ‘A’, dawa za minyoo na upimaji hali ya lishe”, alisema Juma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.