HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inaendelea kuondoa kero ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shule, kwa kujenga miundombinu ya elimu. Mojawapo ni katika shule shikizi ya Chiwondo iliyopo kata ya Nala.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi katika hafla fupi ya kufungua madarasa mawili yaliyojengwa na mbunge wa jimbo la Dodoma mjini Mhe. Anthony Mavunde, tukio lililofanyika katika shule shikizi Chiwondo na kuongozwa na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mheshimiwa Selemani Jafo.
Kunambi alisema kuwa Halmashauri yake imetenga takribani milioni 75 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule shikizi ya Chiwondo. “Awamu ya kwanza tumeleta milioni 17, zinajenga vyoo matundu 12 na madarasa yanayoendelea kujengwa yakikamilika yatakuwa na tiles. Fundi wa hapa ninampongeza anafanya kazi nzuri” alisema Kunambi.
Katika paa za shule hiyo zitaezekwa bati za rangi ili wananchi wafuate lile agizo la Jiji la Dodoma. “Jiji hili tumetengeza ‘clusters’ ya rangi za mabati, kwamba kila Kata ina rangi yake na ndugu wananchi mtuunge mkono, bati sasa ni bei nafuu” alisisitiza Kunambi.
Kuhusu jengo la utawala, Mkurugenzi huyo alisema kuwa Halmashauri yake itajenga jengo la utawala kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021. “Lakini haitoshi, tutajenga nyumba za walimu hapa, walau tuanze nayo moja kwa mwaka wa fedha 2020/21 ili walimu wetu wanaosafiri takribani kilometa 20 wasipate tena adha hiyo” alikazia Mkurugenzi huyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.