WATANZANIA wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujifunza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika shughuli za kilimo na mifugo kwa lengo la kukuza uchumi kupitia shughuli za kilimo na mifugo kibiashara na kuboresha usalama wa chakula.
Wito huo umetolewa na mkuu wa idara ya kilimo, umwagiliaji na ushirika wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Yustina Munishi (pichani juu) alipokuwa akiongelea maandalizi ya maonesho ya shughuli za kilimo na mifugo ya Nanenane yatakayofanyika katika viwanja vya Nanenane eneo la Nzuguni jijini Dodoma.
Munishi amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imedhamiria kuwaonesha watanzania matumizi ya teknolojia mbalimbali za kuwasaidia kukuza uchumi kupitia shughuli za kilimo na kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara na kuboresha usalama wa chakula. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma tumejipanga kuleta mabadiliko kupitia kilimo na kukifanya kilimo kiwe kibiashara, katika eneo letu la banda la Nanenane tumeweka mfumo wa umwagiliaji maji kwa njia ya matone ili watanzania waweze kujionea matumizi ya maji kidogo katika shughuli za kilimo.
Amesema kuwa katika kuonesha teknolojia hizo, zitahusisha matumizi yake katika mazao ya bustani. “Unajua mazao ya bustani ni mazao yenye thamani kubwa sana. Mfano, vitunguu, tutaonesha teknolojia ya kuzalisha vitunguu kwa njia bora na kupata tija. Ukizalisha vitunguu kwenye ekali moja unaweza pata mavuno tani 19 hata na zaidi” alisema Munishi.
Mkuu huyo wa Idara ya kilimo, umwagiliaji na ushirika alisema kuwa Halmashauri inataka kuwainua wananchi kupitia kilimo cha mbogamboga kibiashara. “Katika banda la Jiji la Dodoma, wananchi watafundishwa kulima kibiashara chainizi, kabichi, spanishi, bilinganya, sukumawiki, karoti na mazao mengine mengi. Mazao haya yanaonesha jinsi mwananchi anavyoweza kukuza kipato chake. Tayari wananchi wa maeneo ya Ihumwa, Kikombo na Matumbulu wanazalisha mbogamboga kwa kiwango kikubwa na kuuza nje ya Wilaya ya Dodoma. Haya ni mafanikio makubwa katika dhana ya kukuza uchumi kupitia kilimo” alisema Munishi kwa furaha.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilishika nafasi ya kwanza kwa Halmashauri zote nane za Mkoa wa Dodoma katika maonesho ya Nanenane mwaka 2019.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.