VITUO 59 vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoa elimu na hamasa juu ya unyonyeshaji maziwa ya mama na ulishaji watoto wadogo katika maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama duniani.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Eva Semeni Juma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama duniani ofisini kwake leo.
Juma alisema “Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na wadau tunaadhimisha maadhimisho haya kila mwaka. Miongoni mwa mambo tunayofanya ni kuhamasisha jamii kupitia vyombo vya habari hasa redio za ndani ya Jiji, kuelimisha dhana ya wiki ya unyonyeshaji na ulishaji watoto wadogo”. Kupitia vituo 59 vyenye huduma ya kliniki ya mama na mtoto, kina mama wenye watoto chini ya miaka mitano wanapata elimu hiyo tangu tarehe 1-7 mwezi Agosti, 2019, alisema. Alisema kuwa katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, wataalam wa Halmashauri wamejiandaa vizuri na wanatoa elimu hiyo vizuri.
Afisa Lishe huyo alielezea faida za unyonyeshaji maziwa ya mama na kusema kuwa maziwa hayo ni mlo kamili na lishe bora kwa mtoto. “Maziwa ya mama yana virutubisho vyote vinavyohitajika kwa mtoto kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo na kuendelea hadi miaka miwili” alisema Juma.
Faida nyingine ya unyonyeshaji maziwa ya mama alizitaja kuwa maziwa hayo yanawezesha ukuaji wa mtoto na kumuepusha na kudumaa na kukua kwa ubongo na kumkinga dhidi ya maradhi. Maziwa hayo husaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya mama na mtoto kupitia unyonyeshaji.
Ikumbukwe kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani kwa mwaka 2019 inasema “tuwawezeshe wazazi kufanikisha unyonyeshaji”. Kwa pamoja wazazi wote wawili wana umuhimu katika kufanikisha unyonyeshaji sahihi wa maziwa ya mama.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.