HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inatarajia kutoa mikopo ya Shilingi milioni 400 kwa vikundi vya wajasiriamali Wanawake, Vijana, na Walemavu kuanzia mwishoni mwa mwezi Septemba, 2018.
Hayo yameibainishwa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana wa Jiji hilo Mufungo Manyama wakati akitoa maelezo kwa Wananchi wa Kata ya Iyumbu na Dodoma Makulu mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi aliyekuwa katika ziara ya kikazi kwenye Kata hizo jana Septemba 4, 2018.
Manyama alisema, fedha hizo zitatolewa kwa vikundi vilivyosajiliwa na vitakavyoomba mikopo hiyo, huku akitoa wito kwa Wanawake, Vijana, na Walemavu kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili wafaidike na fursa hiyo.
“Mkishaunda kikundi chenu fikeni Ofisi ya Maendeleo ya Jamii ili tuwasajili na kuwatambua, pia tutawashauri kuhusu kiwango cha mkopo kulingana na miradi yenu kwa sababu mikopo hii ina marejesho ya kila mwezi lakini haina riba kabisa” alifafanua Manyama.
Mkuu wa Wilaya Katambi anafanya ziara ya kikazi katika Kata mbalimbali za Jiji la Dodoma kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za Wananchi na kazitafutia ufumbuzi wa papo hapo huku akiwa ameambatana na wataalam mbalimbali wa Jiji na taasisi nyingine ikiwemo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala ya Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi, na Magereza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.