Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Arusha zimebuka vinara wa ukusanyaji mapato ya ndani kwa robo ya kwanza ya mwaka wa 2018/19 (kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba).
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri zote nchini kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2018/19.
Waziri Jafo amebainisha kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongoza kwa kukusanya mapato ghafi yaani Fedha nyingi kuliko Halmashauri zote nchini; Jiji la Dodoma limekusanya kiasi cha shilingi Bilioni 14.4 kati ya bajeti yao ya kukusanya shilingi bilioni 68. Makusanyo hayo yamefikia kiasi cha asilimia 21 ya malengo waliyojiwekea.
Halmashauri ya Jiji la Arusha imeongoza kwa kukusanya vizuri kiasilimia na imefanikiwa kukusanya mapato yao kwa asilimia 26 ya malengo waliyojiwekea. Hii inamaanisha Jiji la Arusha limekusanya kias/i cha shilingi bilioni 4.1 kati ya shilingi bilioni 15.6 ya malengo yao ya makusanyo kwa mwaka wa Fedha 2018/19.
"Ieleweke wazi kuwa Jiji la Arusha ndi lililofanya vizuri kimakusanyo kwa mujibu wa asilimia lakini Jiji la Dodoma ndio lililokusanya fedha nyingi zaidi kuliko Halmashauri zote nchini Tanzania" alisema Waziri Jafo.
Aliongeza kuwa kwa upande wa Halmashauri za Manispaa iliyofanya vizuri zaidi ni Manispaa ya Musoma na kwa Halmashauri za Mji zimeongozwa na Halmashauri ya Mbinga na upande wa Halmashauri za Wilaya zimeongozwa na Halmashauri ya Kisarawe.
Mheshimiwa Waziri Japo alisema kuwa kwa makusanyo hayo ukiyaweka Kimkoa, basi Mkoa wa Simiyu unaongoza ukifuatiwa na Manyara, Lindi, Mara, Pwani, Arusha, Njombe, Dodoma, Mwanza na kisha Geita.
Waziri alisema Halmashauri zilizofanya vibaya zaidi kwa kukusanya chini ni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Mji wa Nanyamba, Wilaya za Nanyumbu, Newala, Tandahimba, Songea, Madaba, Rorya na Morogoro.
Kwa upande wa Mikoa iliyofanya vibaya kwa kukusanya mapato kidogo ni Mkoa wa Mtwara, Ruvuma na Kigoma. Waziri Jafo aliwakumbusha viongozi wanaohusika kuwa ukusanyaji wa mapato ndio kitakuwa kigezo cha kupimwa katika utendaji wazi wao, hivyo kila mtu ajitathmini kulingana na mapato ya Halmashauri au Mkoa wake.
Kwa mwaka wa Fedha 2018/19 Halmashauri zilipangiwa kukusanya shilini bilioni 735.6 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani; hadi kufikia tarehe 30/09/2018 Halmashauir zilikusanya jumla ya shilingi bilioni 143.6 sawa na asilimia 20 ya makisio ya mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2017/18 Halmashauri zilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 687.3 na hadi kufikia Septemba 30 mwaka 2017 ziliweza kukusanya shilingi bilioni 126.8 sawa na asilimia 18 ya makisio ya mwaka. "Kutokana na takwimu hizo inaonesha kwamba Halmashauri zimeongeza wingi wa mapato kwa kiasi cha shilingi 16.7 na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka kwa asilimia 2" alisema Mhe. Waziri Jafo.
Chanzo: Tovuti ya OR-TAMISEMI
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.