Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kinara wa tuzo na zawadi mbalimbali kwenye maonesho ya kimataifa ya Nanenane kutokana na kufanya vizuri katika maeneo mengi na kuwa kivutuo kwa wageni waliotembelea maonesho hayo.
Katika tuzo na zawadi zilizotangazwa mbele ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliibuka mshindi katika vipengele sita vya mashindano ya Nanenane.
Katika kipingele cha zawadi za wakulima bora kitaifa Kanda ya Kati iliyotolewa na Bodi ya Pamba, Dafalas Wadaa kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma alizawadiwa zawadi ya Trekta.
Kipengele cha wafugaji bora, mshindi wa kwanza aliibuka John Nassar kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuzawadiwa mitamba miwili yenye thamani ya shilingi 9,000,000, mashine ya kukamua yenye thamani ya shilingi 2,300,000 na fedha taslimi shilingi 18,700,000.
Maeneo mengine ambayo Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliibika kidedea ni eneo la wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa ambapo wafugaji John Nassar aliibuka mshindi wa kwanza na kupata zawadi ya shilingi 2,500,000 na Viola Kweka, mshindi wa pili na kupata zawadi ya shilingi 2,000,000. Kwa wafugaji wadogo wa mbuzi wa nyama, Venderine Liakurwa pia wa Dodoma Jiji aliibuka mshindi wa pili na kupata zawadi ya shilingi 1,000,000.
Eneo la wafugaji wadogo wa mbuzi wa maziwa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilitoa washindi wa kwanza na wa pili mtawalia. John Nassari aliyepata zawadi ya shilingi 1,500,000 na Caroline Shayo aliyepata shilingi 1,000,000.
Kwa washindi katika mikoa ya Dodoma na Singida, Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza ikizitangulia Halmshauri za Wilaya ya Kondoa na Mpwapwa za Mkoa wa Dodoma.
Maonesho ya Nanenane mwaka 2024 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Chagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.