HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Kilimo ya Kimataifa ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi (IITA) kama mkakati wa kutoa elimu ya kilimo himilivu kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuwahikikishia wananchi uhakika wa chakula.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Yustina Munishi wakati akihitimisha ziara ya siku ya wakulima katika kata ya Hombolo Bwawani jijini hapa.
“Halmashauri ya Jiji la Dodoma itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi ya kilimo ya kimataifa ya mabadiliko ya tabia ya nchi (IITA) katika kutoa elimu juu ya kilimo himilivu kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.” Alisema kuwa kilimo hicho kinawasaidia wakulima kupata mazao mengi wakati mkulima hatumii nguvu nyingi katika uzalishaji wa mazao.
Munishi alisema kuwa wakulima wanapaswa kuzingatia mafunzo kwa malengo ya sasa na ya baadae kwa sababu kilimo ni uti wa mgongo. Alisema kuwa kupitia mafunzo hayo, mkulima anaweza kujikwamua kimaisha kwa kufanya kilimo cha kibiashara kupitia mbinu mbadala za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Akiongelea muendelezo wa mashamba darasa katika Jiji la Dodoma, alisema “Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejipanga kuhakikisha kwamba mashamba darasa yanakuwepo maeneno yote ya kata ambazo ni za kilimo. Tunazo kata 24 za kilimo na tumeweza kuchukuwa kwanza maafisa kilimo wetu wote kuwaleta kwenye ziara ya mafunzo katika shamba darasa lililopo Hombolo Bwawani, lakini katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021 / 2022 tumetenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa mbegu” alisema Munishi.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa kata ya Hombolo Bwawani, Paschal Sabunyoni alisema kuwa mafunzo kupitia shamba darasa hayakuwepo awali. Kupitia Halmashauri ya Jiji la Dodoma uanzishaji wa mashamba darasa umesaidia katika kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kufanya kilimo himilivu.
“Mwanzo wakulima walikuwa wanaeleza kuwa walikuwa hawazifahamu njia vizuri. Lakini kupitia shamba darasa wamejifunza mengi katika uandaaji wa mashamba, utumiaji wa mbolea na maandalizi ya vifaa katika kilimo kulingana na aina ya mazao, pia utumiaji wa mbegu zilizo bora” alisema Sabunyoni.
Ziara ya siku ya wakulima kata ya Hombolo Bwawani jijini Dodoma ilifanyika katika Mtaa wa Hombolo Bwawani B, ikiongozwa na Mkuu wa idara kilimo, umwagiliaji na ushirika wa Jiji la Dodoma, wataalamu kutoka taasisi ya IITA, Diwani wa Kata ya Hombolo Bwawani, na viongozi waandamizi wa Kata hiyo na wakulima.
Mkuu wa idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Yustina Munishi akiongea na mwandishi wetu mara baada ya ziara ya kutembelea shamba darasa.
Shamba darasa lililotembelewa na wataalam wa kilimo lililoko Mtaa wa Hombolo Bwawani B Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.