Na. Halima Majidi, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma katika kuhakikisha inaimarisha na kukuza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo yake na nchi kwa ujumla imeainisha miradi ya kuingia ubia na kushirikisha sekta binafsi na za umma.
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kupitia mapendekezo ya rasimu ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2025/2026, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Prof. Davis Mwamfupe, alisema kuwa halmashauri imekuja na mkakati mpya wa kujiweka tayari kwa kufanya miradi kwa ubia kupitia mfumo wa ushirikishaji sekta binafsi na sekta ya umma (PPP).
Prof. Mwamfupe alisema kuwa miradi mingi imewekwa katika masoko ili kuweza kuita na kuvutia sekta binafsi ili waweze kushiriki na kuwekeza katika miradi hiyo. “Kwa kuangalia miradi ambayo tulikuwa nayo kipindi cha nyuma na kwa kujifunza kutokana na hiyo tumepata tabu sana kukamilisha miradi miwili ya hoteli. Kwahiyo, tumeweka mkakati mpya wa kushirikisha sekta binafsi na za umma ili kurahisisha ufanisi wa miradi hiyo”, alisema Prof. Mwamfupe.
Aidha, Prof. Mwamfupe alisema kuwa wamefanikiwa kuanzisha kampuni Special Purpose Vehicle (SPV) ambayo ni chombo cha kuendesha miradi ambayo inahusiana na biashara kwa lengo la kutanua wigo wa mapato. Aliongeza kuwa “majukumu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma si sana kufanya biashara. Lakini tunajikuta tunamiradi inayofanya biashara ili kuondoa ukinzani wa namna hiyo tukasisitiza kuwa na mfumo huo pale tunapokuwa na miradi ambayo inaingiza fedha. Pale tunapokuwa na miradi ambayo ubunifu wake unahitaji utaalamu uliopo nje ya uwezo wetu ndio maana tukaona SPV haikwepeki” alisema Prof. Mwamfupe.
Sambamba na hilo, alisema kuwa serikali imeweka adhma ya kuanzisha mji katika eneo la Hombolo Bwawani ikiwa ni katika muendelezo wa mipango miji wa 2019-2039. “Eneo lile lina mandhari nzuri. Hivyo, kutenga maeneo na kujenga mji wa kisasa wenye miundombinu bora na huduma muhimu kwa lengo la kuvutia wageni pamoja na kukuza sekta ya utalii. Tunadhani masaki ya Dodoma itakuwa uekekeo wa namna hiyo”, alisema Prof. Mwamfupe.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Makole, Omari Haji Omari, alisema anaupongeza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuweka mkakati wa ujenzi wa mji mpya wa kipekee Hombolo Bwawani kwasababu sehemu hiyo itawasaidia watu kupata mahitaji yao ya muhimu. “Mtu hatakuwa na sababu ya kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kwaajili ya kufurahi yaani 'kuenjoy' badala yake ataenda Hombolo Bwawani” alisema Omari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.