Na. Asteria Frank, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepanga kukusanya kiasi cha shilingi 1,902,895,000.00 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato katika Soko la wazi la Machinga ili kuweza kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko wakati akisoma taarifa ya uendeshaji wa Soko la wazi la Machinga kwa Kamati kudumu ya Bunge ya Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa iliyofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya soko hilo lililopo eneo la Bahi Road jijini Dodoma.
Dkt. Sagamiko alisema kuwa ujenzi wa soko hilo uligharimu kiasi cha shilingi 9,529,747,200.66. Kati ya fedha hizo shilingi 6,529,747,200.66 ni mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji, shilingi 2,500,000,000.00 ni ruzuku kutoka Serikali kuu na shilingi 500,000,00.00 ni fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko -19 na kuwa soko limekamilika na tayari linatumika.
“Kwa mujibu wa usanifu soko linatarajiwa kubebea wafanyabiashara wadogo 3,034. Hata hivyo, wakati wa utekelezaji soko limekuwa na uwezo wa kubeba wafanyabiashara 2,553 ambapo wamegawanywa katika zoni 10 ambazo ni A, AB, B, BC, C, D, DE, E, EF na F. Kutokana na ongezeko la wafanyabiashara wadogo katika soko hili ililazimika kutengwa kwa eneo la mbele ya soko na pembezoni ili kuweza kubeba wafanyabiashara 100 mpaka 200 ambao hupanga biashara zao katika eneo maalumu ndani ya soko nyakati za jioni na hupaswa kuchangia kiasi cha shilingi 500.00 kwa siku kama gharama ya usafi na kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Juni, 2024, soko hili limeweza kukusanya kiasi cha shilingi milioni 460 katika shilingi bilioni 1 iliyokasimiwa sawa na asilimia 46 ya lengo” alisema Dkt. Sagamiko.
Alisema kuwa ujenzi wa soko hilo umeliweka Jiji la Dodoma katika mandhari safi na kurahisisha shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira. Ujenzi huo umerahisisha utoa wa huduma za msingi kwa wafanyabiashara. “Halmashauri ili kuweza kufikia lengo la bajeti iliyowekwa tayari imeandaa mikakati ifatayo. Tayari halmashauri iemshatengeneza tenda na imempata mzabuni atakayehusika kukusanya ushuru na kodi kwa wafanyabiashara wote ndani ya soko. Halmashauri inaendelea na zoezi la kuelimisha wafanyabiashara kupitia viongozi wao juu ya ulipaji ushuru na utunzaji wa miondombinu ya soko. Kwa kushirikiana na viongozi wa soko halmshauri imeadaa kutatua changamoto mbalimbali zinapojitokeza kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara kwa kundi hili” alisema Dkt. Sagamiko.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Tamisemi ilifanya ziara ya kawaida ya kutembelea na kukagua maendeleo ya uendeshaji wa Soko la wazi la Machinga lililojengwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa zaidi ya shilingi bilioni tisa likiwa na uwezo wa kubeba zaidi ya wafanyabiashara 3,000.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.