HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imejipanga kuongoza katika usafi wa mazingira kwa upande wa Halmashauri za Majiji kutokana na nafasi yake ya kimkakati nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akielezea mipango ya Jiji hilo kuhusu usafi wa mazingira muda mfupi kabla ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kuzindua kituo cha kupokelea mifuko ya plastiki kilichopo katika kata ya Uhuru.
Kunambi alisema kuwa, Halmashauri ya jiji la Dodoma imejipanga kuongoza katika upande wa Majiji nchini kwani Dodoma ni Makao Makuu ya nchi, hivyo suala la usafi ni agenda ya kudumu.
“Halmashauri ya Jiji la Dodoma tumejipanga vizuri ambapo tumekuwa tukitoa elimu ya usafi wa mazingira na madhara ya mifuko ya plastiki kuanzia ngazi ya mitaa, kata hadi wilaya” alisema Kunambi.
“Mheshimiwa mkuu wa Wilaya, Halmashauri ya Jiji la Dodoma tunaenda kuongoza na kuwa wa mfano Tanzania, tumekuwa na utamaduni wa kuongoza katika mapato, usafi, afya, elimu, sababu kubwa sisi wote ni vijana...tunafikiria miaka 50 ijayo ya siyo miaka 50 iliyopita” alisema Kunambi.
Aidha, aliwapongeza wakazi wa Jiji la Dodoma kwa utulivu na ushirikiano wanaoendelea kumpatia katika kutekeleza majukumu yake.
Akiongelea juu ya utii wa sheria, aliwataka wananchi wa Jiji hilo kutii sheria bila shuruti na kusema kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mtu.
“Katika nyumba yako au eneo unalofanyia shughuli zako, hakikisha hakuna mfuko wa plastiki unaozagaa” alisema Kunambi.
Kuhusu taasisi zinazokaidi kutoa tozo kwa ajili ya ubebaji taka na usafi wa mazingira, mkurugenzi huyo alionesha masikitiko yake kwa baadhi ya taasisi hizo na kusema zinakwamisha juhudi za usafi wa mazingira. “Wengine wanafikiria usafi siyo sehemu yao. Zipo taasisi kubwa hazilipi tozo ya usafi wa mazingira. Tusimame pamoja ili kusafisha jiji letu” aliongeza Kunambi.
Aidha, Mkuu wa idara ya Mazingira na udhibiti taka ngumu katika jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa Halmashauri hiyo ilijikita katika kutoa elimu kuanzia ngazi ya Mtaa, Kata na Wilaya juu ya katazo la serikali la matumizi ya mifuko ya plastiki na kuelezea mifuko mbadala. Alisema kuwa elimu hiyo ilitolewa kupitia njia mbalimbali za mawasiliano kuanzia mitandao ya kijamii hadi vituo vya runinga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.