Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya JUZA, Nasibu Kitabu kwa kushirikiana na Kampuni ya Global Waste Solutions watambulisha mradi wa uchakataji na urejeshaji wa taka kwa Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kupunguza kiwango cha taka zinazopelekwa katika Dampo la Chidaya.
Aliyazungumza hayo katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri na kusema kuwa taasisi hiyo imejikita katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira pamoja na kutoa elimu kwa vijana wanaofanya kazi ya kuzoa taka. “Kwasasa tupo katika Jiji la Dodoma na tumeungana na Global Waste Solutions kufanya hii kazi ili kupunguza kiasi kikubwa cha taka kwenda dampo ifikapo mwaka 2027. Yote hii ni kuweza kuifundisha jamii namna ya kutenganisha taka ili tuweze kuiokoa jamii yetu na changamoto zitokanazo na utunzaji na utupaji holela wa taka” alisema Kitabu.
Aliongeza kuwa Jiji la Dodoma limekuwa kwa kasi na ndipo ilipo sura ya nchi. “Jili la Dodoma ni fahari ya watanzania, tumeona ni vema tukaanzia hapa ili kuweka mji safi lakini pia mazingira ya wananchi yawe salama. Elimu nzuri itasaidia jamii kujua namna ya kutenga taka kwasababu zipo taka nyingine zinatumika kutengeneza mbolea na vitu vingine” aliongeza Kitabu.
Alisema kuwa mradi huo utajikita katika maeneo ya kuhamasisha jamii kutenganisha taka katika ngazi ya kaya na taasisi na kuhakikisha taka zinazoweza kutumika tena ziweze kurejeshwa kiwandani. Pia utajikita katika kutenganisha taka ngumu kama plasitiki na taka oza kama vile mabaki ya vyakula.
Nae, Mtaalam na Msimamizi wa Udhibiti Taka ngumu Global Waste Solutions, Amir Amir alisema kuwa mradi huo wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira umejikita katika maeneo matatu ya Jiji la Dar es Salaam, Jiji la Dodoma na Moshi. “Mradi huu kwa Jiji la Dodoma ni muhimu kwasababu hapa ndio makao makuu ya nchi na tutaanzisha vituo vya kudhibiti taka ngumu ikiwemo plastiki na karatasi na tutaanzisha kituo cha uchakataji wa mabaki ya taka oza ikiwemo vyakula na matunda yanayoharibika katika masoko na majumbani. Kwahiyo, tutatengeneza mbolea ya asili na wadudu watakaotumika kama protini mbadala kwaajili ya vyakula vya mifugo” alisema Amir.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa Taka ngumu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alieleza kuwa, wamepokea utambulisho wa mradi wa Taasisi ya JUZA kwa ushirikiano na Global Waste Solutions wa uchakataji na urejeshaji wa taka. “Sisi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, eneo hili ni moja ya maeneo ya kimkakati ambao tulijiwekea kuwa tutashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha tunarejesha taka, tunatenganisha taka na kutoa elimu kwa wananchi wafahamu namna ya kutenganisha taka” alifafanua Kimaro.
Alimalizia kwa kutoa ahadi ya kushirikiana na wadau hao katika kuhakikisha wananchi wa Dodoma wananufaika na uwepo wa mradi huo wa kuliweka jiji safi na salama. “Kipekee kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, nichukue nafasi hii kuwakaribisha sana nyie wadau wetu, tunawaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kwamba huu mradi katika kipindi cha miaka miwili unatekelezwa na unakuwa na manufaa kwa wananchi wa Dodoma na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kiuchumi” alimalizia Kimaro.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.