HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeanzisha kampeni ya upandaji miti katika jitihada yake za kulifanya jiji hilo kuwa la kijani na mahali salama pa kuishi watu wote.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akiwasilisha utangulizi wa Mpango Kabambe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma mbele ya kamati ya uwekezaji ya Bunge la Jumuiya ya Madola kanda ya Afrika waliotembelea jiji hilo kuangalia fursa za uwekezaji katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma jana.
Kunambi alisema kuwa katika kulifanya Jiji la Dodoma linakuwa mahali salama zaidi pa kuishi, Halmashauri yake imeanzisha kampeni kubwa ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali. Alisema kuwa katika kutekeleza kampeni hiyo vikao vya maamuzi vimepitisha kuwa kila kaya itakuwa na wajibu wa kupanda angalau miti mitano kuzunguka eneo la kaya hiyo. “Tunataka ndani ya miaka minne ijayo Jiji la Dodoma liwe la kijani” alisema Kunambi. Aidha, aliongeza kuwa jiji hilo linajipanga kukabiliana na changamoto ya menejimenti ya taka ngumu. Alisema kuwa dhamira ya jiji hilo ni kufikia uwezo wa kutenganisha taka ngumu na taka nyingine na kufanya mchakato wa kuzichakata kuwa rahisi.
Akiongelea eneo la uwekezaji, Mkurugenzi huyo aliwakaribisha wabunge hao kuwekeza katika kilimo cha zabibu na uchakataji wake. “Katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma mnakaribishwa kuwekeza katika kilimo cha zabibu na mazao mengine” alisema Kunambi. Vilevile, alisema kuwa Halmashauri hiyo imeandaa na kutenga maeneo mengine kwa ajili ya uwekezaji katika viwanda kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Akiongelea miundombinu, alisema kuwa barabara za ndani ya jiji zinaendelea kujengwa kwa ajili ya kuunganisha na kuboresha miundombinu hiyo kwa wananchi. Alisema kuwa nia ya jiji hilo ni kuunganisha mtandao wa barabara, reli na anga. “Uwanja wa Ndege wa Msalato unatarajiwa kujengwa ndani ya muda mfupi. Usanifu wake umekamilika na kazi ilifanywa na kampuni kutoka nchini Tunisia. Kwa mujibu wa Mpango kabambe wa Halmashauri ya Jiji, tutaunganisha uwanja wa Ndege uliopo karibu Km 30 kutoka mjini kati na reli ya umeme ya kisasa (SGR) itakayotokea Dar es Salaam kuja Dodoma. Mradi unaoendelea na unatarajiwa kukamilika mwaka 2021. Baada ya kukamilika mtu atakuwa na uwezo wa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa kutumia masaa matatu pekee” alisema Kunambi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.